MASHUJAA YAIKUNG’UTA FOUNTAIN GATE 3-0 KIGOMA

WENYEJI, Mashujaa FC wameibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara leo Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma. Mabao ya Mashujaa FC yamefungwa na Jaffar Kibaya dakika ya 32 kwa penalti, Idrisa Stambuli dakika ya 49 na Seif Karihe dakika ya 77 na kwa ushindi huo wanafikisha pointi 27 na kusogea nafasi ya tisa, ikiizidi tu wastani wa mabao KMC baada ya wote kucheza mechi 24. Kwa upande wao Fountain Gate baada ya kupoteza mchezo huo wanabaki na pointi zao 28 nafasi ya nane baada ya kucheza mechi 25 kadhalika. Ligi Kuu inashirikisha timu 16 na mwisho wa msimu mbili zitashuka Daraja na mbili nyingine zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu. Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu ya Championship kujaribu tena kubaki Ligi Kuu.