HIVI UMEWAHI KUJIULIZA HASA KILE ANACHOKITAKA ZAHERA YANGA!






NA SALEH ALLY
UNAPOITAJA Klabu ya Yanga kuhusiana na wafanyakazi wake wa kigeni, Wakongo watatu ni gumzo na kila mmoja ana la kwake ambalo halifanani na mwenzake.

Mmoja ni Klaus Kindoki ambaye ni kipa namba tatu wa Yanga kwa sasa. Mgeni ambaye ni kipa namba tatu, jambo halijawahi kutokea katika nchi yoyote.

Kindoki amekuwa gumzo kubwa sana kutokana na hilo, lakini bado benchi la ufundi limeendelea kumuamini, jambo ambalo binafsi napingana nao. Yanga haiwezi kusajili kipa wa kimataifa aje akuze kiwango wakati akilipwa fedha nyingi kuliko wazawa ambao Yanga ina uwezo wa kuwalipa nafuu na kuwakuza.

Wa tatu ni Heritier Makambo. Huyu jamaa ni mshambuliaji na sasa ameanza kuudhihirishia umma wa wapenda mpira kwamba yeye ni hatari sana tofauti na wengi walivyokuwa wakiamini kwamba hawezi.

Makambo hana nyota ya karibu kuwavutia mashabiki. Huenda ni kwa kuwa si mtu mwenye mbwembwe sana. Lakini unapozungumzia kazi yake, ni bora na anaijua.

Kutofunga kwa muda kwa mshambuliaji, inatokea. Kuna kipindi cha ukame wa mabao na hata ukimuuliza mshambuliaji yeyote atakwambia kiliwahi kumtokea na uvumilivu, kuendelea kujituma na kutaka kufanikisha huwa kunabadilisha mambo.

Sasa Makambo, anaongoza kwa kuwa na mabao 11 katika Ligi Kuu Bara. Sahihi kwa mshambuliaji anayetokea nje kuwa mkali katika ufungaji na huo ndio msaada wake kwa timu.

Mtu wa tatu hapa ni kocha, huyu ni Mwinyi Zahera. Raia wa DR Congo ambaye pia ni kocha msaidizi wa Timu ya Taifa ya DR Congo.

Zahera amekuwa kocha aliyeshangaza sana kama utafuatilia. Kwa wale wanaomfahamu si kocha mdogo na ndio maana aliaminika kuwa mmoja wa wanaounda Benchi la Ufundi la Chui wa DR Congo. Si jambo dogo kwa kuwa nchi hiyo na rundo la hazina ya makocha.

Jiulize kwa nini Zahera alikubali kuja Yanga ambayo ilionekana wazi kwamba ina hali ngumu ya kiuchumi. Huenda hakujua, lakini baada ya muda mfupi aliiona hali kwa kuwa hata wakati aliyemrithi anaondoka ambaye ni George Lwandamina raia wa Zambia, hakuwa amelipwa fedha zake.

Baada ya muda mfupi Zahera kukaa Yanga, aliiona hali halisi na namna mambo yalivyokuwa. Hali ikawa mbaya na mambo yakazidi kuwa hovyo.

Pamoja na hivyo, Zahera ameendelea kubaki Yanga bila ya woga wala kuchoka. Jiulize kwa kocha kama yeye, anaendelea kusubiri nini ndani ya Yanga.

Kitu ambacho unaweza kujifunza kwa Zahera ni kocha ambaye anaangalia mafanikio zaidi kuliko fedha. Hakika wengi wetu tumekuwa tukiangalia fedha zinazoingia kwanza baada ya kazi na si mafanikio. Wakati mafanikio yanamsaidia mtu kupata fedha nyingi zaidi kuliko angeanza kuangalia fedha kwanza.

Zahera ametoa Sh 150,000 kwa kila mchezaji wake mara baada ya mechi ya mwisho ya mwaka 2018 dhidi ya Mbeya City na wao kushinda kwa mabao 2-1.

Zahera ambaye alisafiri kwenda Ufaransa alikokuwa akikabiliwa na matatizo ya kifamilia, alisikika akiwaomba wanachama na mashabiki kuichangia Yanga. Mwisho akasema hivi: “Kama kuna ile itapungua, mimi nitaongezea.”

Kocha Zahera anataka nini Yanga? Badala ya kupata fedha aendeshe maisha kupitia kazi yake. Yeye anailipa kazi yake? Huyu ana akili nyingi sana na ana mapenzi makubwa na kazi yake.

Mkongoman huyu zaidi anaangalia mafanikio na huu ni msukumo mkuu kutokana na mapenzi ya juu aliyonayo. Kama kweli Yanga itafikia kuchukua ubingwa, jambo ambalo bila ubishi Zahera analitaka ili kutengeneza CV yake, basi Zahera ataandika historia hapa nyumbani.

Wako makocha waliwahi kufanya hivi kama Patrick Phiri wa Simba akitokea Zambia na marehemu, Jack Chamangwana, difenda wa zamani wa Kaizer Chiefs na timu ya Taifa ya Malawi, lakini bado hawakufikia hapa kwa Zahera.

Binafsi naendelea kujifunza na kuhifadhi rekodi na Zahera anazidi kunifundisha kwamba penda kazi yako kwanza, fedha zitafuatia. Acha Tuone mwisho atapata nini.



Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA