SIMBA HUKU MLIPOFIKIA, NI VITENDO ZAIDI BADALA YA MANENO
Na Saleh Ally
KAMA tungesikiliza maneno, basi Simba isingepiga hatua na kufikia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hii si hatua ndogo hata kidogo kwa klabu za Afrika.
Kuna klabu nyingi kubwa ambazo haujaziona katika hatua hii, angalia Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Al Hilal (Sudan), Zamalek (Misri), CS Sfaxien (Tunisia), Asante Kotoko (Ghana), Enugu Rangers (Nigeria) na nyingine nyingi ambazo pia zina utajiri mkubwa lakini zimeshindwa kufikia hatua hii.
Tukitaka kuwa waungwana, kwanza ni kuwapongeza Simba kufikia hatua hii ngumu ambayo itakuwa changamoto na itazaa mafundisho mengi katika soka nchini.
Pamoja na hivyo, tukitaka kuwa waungwana zaidi, kinachotakiwa ni kuwaambia Simba ukweli na si kuangalia ushabiki. Inawezekana wako wanaopenda ushabiki tunaweza kuwaachia nafasi ya kile wanachokifurahia na sisi tukaangalia njia nyingine sahihi kama wataalamu au wanataaluma ambao tungependa Simba ifanye vizuri zaidi.
Makundi manne ya Ligi ya Mabingwa Afrika yameishapangwa na Simba ambao ni wawakilishi wa Tanzania na Afrika Mashariki, wameangukia Kundi D lenye timu nyingine tatu.
Timu mbili katika kundi hilo zinatokea Afrika Kaskazini, ukanda ambao ndiyo wenye ubora namba moja katika soka hapa nyumbani. Timu iliyobaki inatokea Afrika ya Kati ambao ni ukanda namba tatu kwa ubora Afrika.
Timu mbili za Afrika Kaskazini, Al Ahly ya Misri na JS Soura ya Algeria ambayo sasa itamtumia Mtanzania, Thomas Ulimwengu. Timu hizi zina aina mbili tofauti, Al Ahly inajulikana kwa ukubwa kirekodi, historia na takwimu kwa kuwa ndiyo klabu yenye mafanikio zaidi katika bara hili.
Pale kati kuna AS Vita, vigogo kutoka DR Congo ambao wanajulikana kwa ubora wao ingawa inaonekana huenda wengi wanaamini ni nafuu zaidi ya kukutana na TP Mazembe, jambo ambalo si sahihi.
Simba inatokea Afrika Mashariki, ukanda ambao ni wa chini zaidi kisoka katika Bara la Afrika. Na ndiyo mwakilishi pekee na utaona maana ya ubora wa chini, mara nyingi unatoa timu chache. Wakati mwingine au mara nyingi zaidi hatua ya makundi imekuwa ikipangwa bila ya kuwa na timu kutoka Afrika Mashariki.
KUNDI D
Al Ahly:
Umri wa hii klabu ni miaka 111, hakuna ubishi inajua mengi na ndiyo imechukua ubingwa wa Afrika mara 8, ambayo ni mara nyingi zaidi ya klabu nyingine yoyote.
Imeweka rekodi ya kubeba ubingwa wa Misri mara 40. Kombe la Misri mara 36, Misri Super Cup 10, Cairo League mara 15 na kadhalika. Wanaona hawana hofu na suala la makombe.
Hii haina maana hawafungiki na ukiangalia kumekuwa na udhaifu baada ya kizazi cha akina Mohamed Aboutrika. Miaka kadhaa imepita nilisafiri hadi Cairo nikiwa na Yanga ambao walikuwa wameshinda jijini Dar es Salaam kwa bao 1-0. Kule wakafungwa bao 1-0 na mwisho ikawa mikwaju.
Yanga walishindwa wenyewe kwa kuwa Said Bahanuzi angefunga penalti ya mwisho Yanga ingesonga mbele. Maana yake, hata kwao inawezekana na wakati ule bahati mashabiki hawakuwa wakiruhusiwa.
Simba wakijiandaa na kuacha maneno mengi au kuamini kwa hisia wana kila nafasi ya kupata pointi moja au tatu pale, lakini lazima tuwe wakweli, kazi ya ziada kwa maana ya maandalizi ya wachezaji kimwili kwa maana ya fiziki na kisaikolojia iwe ni asilimia 100.
Ahly ni klabu namba moja Afrika, namba 69 duniani. Huu ni mzigo mzito lakini unaobebeka Simba wakiamua.
JS Soura:
Kule Algeria inajulikana zaidi kama JSS, yaani JS Soura. Hapa Tanzania imeanza kujulikana siku chache zilizopita baada ya kumsajili Ulimwengu.
Hii ni mara yao ya kwanza kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika lakini wanaonekana kuwa wamepania kuwa wakubwa. Si klabu kongwe kwa kuwa imeanzishwa mwaka 2008, sasa ndiyo miaka 10.
Unaweza kuipima hivi, ndani ya miaka 10 katika nchi kama Algeria, tayari imeweza kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika. Maana yake, hii ni klabu ya kuangaliwa kwa jicho la umakini sana.
Simba wanaweza kupata pointi nne hadi sita kama wakiamua. Vizuri kwa kuwa wanaanzia nyumbani, itakuwa mara ya kwanza Soura wanacheza mechi ya namna hiyo. Ugeni wao, Simba wanaweza kuutumia kuhakikisha wanaondoka na kamba mguuni lakini lazima kazi ya uhakika ifanyike.
AS Vita:
Hii pia unaweza kuiita Vita Club. Si ndogo kama wengi wanavyofikiri kwa kuwa mwaka 1973 walikuwa mabingwa wa Klabu Bingwa Afrika ambayo sasa ni Ligi ya Mabingwa. Wamewahi kubeba Kombe la Shirikisho Afrika miaka miwili mfululizo, ambayo ni 2016 na 2017 ambao ni mwaka jana.
Kwa Congo wao ndiyo wanaochuana na TP Mazembe lakini wakionekana ni bora na maarufu zaidi kwa upande wa Kinshasa na Mazembe wanatamba ukanda wa Lubumbashi.
Hatari zaidi ni kwamba wamechukua Kombe la Shirikisho mara mbili mfululizo na inaonyesha walipania kupanda hadi Ligi ya Mabingwa na kuna kitu wanataka kufanya. Bado uwezo wa Simba kuchukua pointi nne hadi sita inawezekana lakini kwa maana ya ugumu, baada ya Ahly, basi ni hawa Wakongo.
Mpira wa Wakongo ni nguvu na kasi. Simba lazima wajiimarishe katika hilo kwa maana ya kiwango cha uimara wa miili yao lakini uchezaji wa akili kuwazuia Wakongo kucheza aina ya uchezaji wao.
Vita imeanzishwa mwaka 1935, inaizidi Simba mwaka mmoja wa kuzaliwa. Ukiangalia mafanikio yake Afrika ni makubwa. Hivyo, Simba inaweza kujipima na kujiandaa mapema.
Maneno ya tunaweza bila vitendo vya maandalizi sahihi, vitaiangusha Simba. Badala yake, maandalizi sahihi kutoka ndani ya mioyo ya wanaoandaa na wanaojiandaa iwe yenye malengo sahihi.
MAKUNDI MENGINE:
KUNDI A
Waydad
Sundowns
Asec Mimosa
Lobi Star
KUNDI B
Esperance
Horoya
Orlando Pirates
FC Platnums
KUNDI C
TP Mazembe
Ismaily
Constantine
Club African
Comments
Post a Comment