SIMBA SAWA AL AHLY WAGUMU, ILA MKIJARIBU INAWEZEKANA


NDANI ya wiki iliyopita, kulikuwa na mambo mengi kwelikweli kwenye medani ya soka ambayo yalitokea. Ndani ya siku saba tu, kuna matukio ya Kombe la SportPesa ambalo kama ilivyo ada Watanzania tumeshindwa kufua dafu kwa kuruhusu ubingwa uende Kenya.

Pia siku hizo kukaibuka hoja ya wachezaji wa Simba kutoroka kambini na mwishowe kabisa tukamaliza kuhusiana na Kombe la Shirikisho (FA) ambalo liliendelea kwa mechi kadhaa. Yote hayo yameenda na hii ni wiki nyingine, kwa hiyo tunayaweka pembeni.

Baada ya kuanza na mambo hayo, sasa narudi kwenye mada yangu. Msafara wa Simba jana jioni uliondoka nchini na kwenda Misri kwa ajili ya mechi yake nyingine ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, wameenda Misri kucheza na vigogo Al Ahly katika mechi nyingine ngumu ya ugenini itakayofanyika Jumamosi hii.

Mechi hii imekuja ikiwa ni wiki chache baada ya kikosi hicho kutoka DR Congo ambapo kilipoteza kwa mabao 5-0, hoja yangu ya msingi ipo hapa. Natambua hali na mawazo ya wachezaji yalivyo baada ya kukutana na kipigo kizito kama hicho.

Ninaelewa fika kwamba fikra za wachezaji hao zitakuwa zimevurugika hasa baada ya mechi ile na AS Vita kwa sababu tu ya kukutana na mvua hiyo ya mabao. Lakini niwaambie kwamba wao ndiyo wameshikilia maamuzi ya kubadilisha kila kitu mbele yao kama tu wakiamua. Ninasema wakiamua kwani ndiyo wanaoshuka uwanjani na kupambana na timu pinzani.

Japo kinadharia inaonekana kama Simba tayari wameshapoteza pambano hili, lakini kwenye suala la soka bado nafasi iko wazi kwa kila timu. Wengi wanaona kama Al Ahly wana nafasi kubwa ya kushinda, siwapingi ila ninataka tu kuwaambia kwenye soka la kisasa mambo hayaendi hivyo.

Sawa wanasema Al Ahly wapo nyumbani na watabebwa na uwanja wao wa nyumbani, lakini niwakumbushe kwamba kiwango cha timu nyingi za Kiarabu wakiwemo hao Al Ahly kwa sasa kimepungua.

Zamani ilikuwa kawaida kwa timu ya Tanzania kwenda huko na kufungwa zaidi ya mabao matano kwenda mbele, lakini kwa miaka ya hapa kati tumeona hata kama ikitokea timu inafungwa basi ni bao moja au mawili tu, tena wakati mwingine timu zikienda sare.

Kutokana na hilo, ninaamini kabisa Simba wana nafasi ya kufanya jambo fulani kama ikitokea wakajipanga vyema pamoja na kutulia na kujua nini wanatakiwa wafanye kwenye mechi hiyo kwa ajili tu ya kupata matokeo yaliyo mazuri.

Ninaamini benchi la ufundi pamoja na wachezaji wenyewe watakuwa wamejifunza kitu kufuatia kipigo cha mechi iliyopita na AS Vita na kama wakitumia kama funzo kwao basi itakuwa na maana kwao kwa kiasi kikubwa.

Vyote ambavyo vilitokea kwenye mechi ile kama vikigeuzwa kwa njia chanya basi kutakuwa na jambo la maana ambalo wanaweza kulifanya na likawapatia matokeo mazuri kwenye mechi hii.

Niwaibie siri kwamba hakuna kisichowezekana kwenye soka la kisasa na haijalishi timu inacheza kwake ama ugenini, kikubwa cha kuzingatia ni kucheza kwa nidhamu na kujua mko uwanjani kwa ajili ya kutafuta nini.

Mwisho nimalizie kwa kuwatakia kila la kheri kwenye mechi hiyo na mtambue kwamba mamia ya Watanzania watakuwa nyuma yenu nyie mkiwa kama vioo vyao kuona mnawapambania na kuwatoa kimasomaso pale mtakaporudi nchini

Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA