HILI LA KUSEMA KILA MMOJA ASHINDE MECHI ZA NYUMBANI NI TATIZO LINALOUA SOKA 'MDOGOMDOGO'


MAUMIVU yanazidi kuwa makubwa kadri siku zinavyozidi kwenda hasa kwa timu ambazo zipo chini kwenye ligi kuu pamoja na uwezo wao kiuchumi kushindwa kuwa bora.

Kwa zile ambazo zina matumaini ya kuendelea na safari kwa imani ni chache kwa sasa kutokana na kila mmoja kutumia nafasi aliyonayo kuona anapata matokeo uwanjani hata kwa njia ambazo sio halali.

Timu nyingi kwa mzunguko huu wa pili zinazidi kuonewa na vigogo wa ligi ambao wanatafuta mafanikio yasiyo halali hasa kwa kuja na tabia ambayo imeanza kuleta matokeo ambayo ni ya ajabu na huwezi kusema kuna haki.

Kwa sasa kumekuwa na mtindo kwenye ligi kwamba kila timu inashinda mchezo wa nyumbani tena kwa mipango na maelekezo kutoka kwa viongozi jambo ambalo naona halipo sawa hasa kwenye soka letu.

Nasema haipo sawa kutokana na ukweli kwamba kutengeneza matokeo kabla ya mchezo hili jambo halikubaliki mamlaka husika kwa sasa namaanisha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapaswa kuwa macho muda wote kuona haya mambo hayatokei tena.

Kumekuwa na mtindo kwa timu nyingi zinapokuwa nyumbani kuwa na mazingira ya kubebwa na pande zote mbili yaani mashabiki ni wa kwao wanakudhoofisha nje ya uwanja na ndani ya uwanja waamuzi nao wanakukandamiza ili usipate matokeo.

Vita kubwa kwa timu kwa sasa ni utendaji wa haki ndani ya uwanja, zipo timu ambazo zinashindwa kupata matokeo haina maana kwamba hazina uwezo hapana bali ni namna ambavyo mazingira yanatengenezwa kwa timu kushindwa kupata matokeo.

Mfano mchezo kati ya Alliance FC na JKT Tanzania utaona namna ambavyo mwamuzi alipeta matukio mengi muhimu kama penalti ya wazi kwa JKT na kukubali kutoa bao ambalo kiuhalisia lilikuwa na utata hasa kutokana na kuwepo na dalili za kuotea.

Hili halipo sawa kwenye soka linaleta ukakasi na kuua ule ushindani ambao ulikuwepo kwenye ligi yetu ambayo bado inasuasua kiuendeshaji kutokana na kukosekana kwa mdhamini mkuu.

Pia mchezo mwingine ni ule kati ya Stand United na Lipuli, mchezo huu ulikuwa ni wa aina yake pale Shinyanga namna ambavyo haikuwa kazi rahisi kupata matokeo kwa wageni Lipuli.

Nikukumbushe tu matokeo ya mchezo wa Alliance na JKT Tazania, Alliance ilishinda kwa bao 1 na ule kati ya Stand United na Lipuli wenyeji Stand United waliibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Sasa hapo utaona namna ilivyo kwa sasa na hii inatokana na mazingira ambayo timu wenyeji wanatengeneza kutokana na kuwa karibu na waamuzi ambao wanasimamia mchezo ukizingatia kwamba jukumu la kuwakarimu ni lao sasa hapo nadhani TFF wanapaswa watazame upya.

Waamuzi wameanza kuwa na tabia ambayo haileti matokeo chanya kwa wageni bali wenyeji wanafaidika na kuwakaribisha wageni na kupata matokeo kwa namna ambavyo wao wanataka jambo ambalo ni hatari kwenye soka letu.

Umakini unahitajika kwa waamuzi katika kutoa maamuzi ambayo yatasaidia kumpata mshindi wa kweli bila kujali ni mwenyeji au la, sheria 17 za mpira ni lazima zizingatiwe bila upindishaji.

Haki ya wanyonge na wapambanaji wa kweli ndani ya uwanja na ipatikane kusiwe na ujanjaujanja wa kutengeneza matokeo kama kisingizio cha kuwa mwenjeji hapana hili halipo sawa.

Yote haya yanatokana na ukata ambao unazikumbuka klabu nyingi kwa sasa pamoja na baadhi ya viongozi ambao si waadilifu kuamua kufanya mambo kinyume na taratibu zilizopo.

Mwamuzi akionyeshwa hela kidogo tu anakubali kupindisha sheria 17 hii haipo sawa inadumaza soka letu na kuua kabisa ushindani ambao ulianza kujitokeza awali.

Ligi imekuwa ngumu kwa timu nyingi ambazo hazina uwezo ama zile ambazo zinakuwa ugenini zinapata taabu kupata matokeo kwa sababu ambazo ukizifuatilia lazima ugundue kwamba kuna kubebana kwenye kutafuta matokeo.

Timu zenye uwezo na zinazojianda kupata matokeo chanya zimeishia kushangaa zinapoteza pointi tatu katika mazingira ambayo kwao si sawa licha ya kupambana ndani ya uwanja.

Hapa majanga ni mengi kwenye hizi mechi za mwisho ni mwendo wa mwenye kisu kikali ndiye ale nyama linaumiza timu nyingi ambazo zinapambana kwa hali na mali kutafuta matokeo chanya.

Timu wenyeji zinawanyonya wageni bila huruma hata kama wana wachezaji bora na wanaweza kupata matokeo hili linapaswa litazamwe kwa ukaribu na mamlaka husika si la kufumbia macho.

Makocha wanabeba maumivu makubwa na hasa kwa mechi ambazo hazirushwi moja kwa moja zinaumiza kutokana na wamuzi kujiona wapo kwenye ulimwengu wao wanafanya vile mbavyo wanahitaji.

Ifike wakati kila mmoja awe na imani na wachezaji wake pamoja na maandalizi kwani mchezo wa mpira hauna uchawi mkubwa zaidi ya maandalizi mazuri ambayo yatasaidia kupatikana timu za kweli ambazo zitashuka daraja na zile ambazo zitabaki.

Maamuzi yakiwa sahihi hata yule ambaye atashuka daraja atajua kwamba alikosea wapi na afanye nini endapo atarejea tena kwenye ligi kupambana ila kwa hali livyo sasa mambo sio shwari.

Tunahitaji kuona tunampata bingwa wa kweli ambaye atasaidia kupeperusha bendera ya nchi kimataifa kwa haki bila dhuluma yoyote ile hiyo itasaidia kuona namna ambavyo kila mmoja anatimiza wajibu wake uwanjani na nje ya uwanja.

Tusisahau hapa ni lala salama kila mmoja anatetea nafasi yake hivyo TFF wasilale watazame namna mwenendo mzima na mchakato wa kutafuta matokeo unavyokuwa hali itakayowapa mwanga wa kujuaa kipi kifanyike kuboresha ligi yetu.

Wachezaji pamoja na viongozi wanaokuwa wenyeji wanapaswa wajue kwamba dunia ya sasa ni kijiji wasifikiri wanavyojificha kwa kivuli cha wenyeji itakuwa rahisi kwao kupata matokeo sio sawa haijengi bali inabomoa kwa wale wenye vipaji na uwezo hawatumii njia ya mkato.

Kila mmoja awe balozi wa haki na acheze kwa kuzingatia kanuni mambo ya rafu za nje ya uwanja si sawa muhimu kutambua kwa kufanya hivyo matokeo yake ni kuwa na timu ambazo hazina uwezo wa kucheza uwanjani bali nje ya uwanja.



Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA