MAKAMBO APOTEZWA VIBAYA


SAHAU kabisa kuhusiana na Emmanuel Okwi, John Bocco na huyu Mzambia anayeitwa Claytous Chama.

Wala usihangaike na Amissi Tambwe, Ibrahim Ajibu au Mrisho Ngassa. Shoo ya Simba na Yanga sasa imehamia kwa watu wawili tu ambao wametumwa Dar es Salaam tena mitaa ya Kariakoo kutafuta noti.

Huku Yanga yupo mtu mtaalam wa kuwajaza, ukizubaa tu kwenye boksi tayari utamkuta kule pembeni akiwajaza na mikono yake. Anaitwa Heritier Makambo. Huku Simba kuna mzee kijicho Meddie Kagere a.k.a MK14. Wote wamefunga idadi ya mabao 12. Sasa sikia balaa la Makambo.

Tathmini ya mabao ya Makambo inaonyesha kuwa jamaa ni bora kwenye kuzifumania nyavu kutokana na uwezo wa kutumia mguu adimu wa kushoto kitu ambacho kimekuwa adimu kwa washambuliaji wengi. Guu hilo limemtofautisha na Kagere ambaye ndiye straika mwiba kwa Simba.

Ubora wa Makambo umeonekana kutokana na kuwa na matumizi makubwa ya mguu wa kushoto katika ufungaji wa mabao matano kati ya 12 aliyonayo.

Straika huyo ametumia mguu wake wa kushoto kufunga katika mchezo dhidi ya Coastal Union (0-1) akifunga bao dk ya 11, Mbeya City (1-2) dk 17, Mwadui FC (1-2) dk 10, Lipuli FC (1-0) dk 10 na JKT Tanzania (3-0) dk 20.

Makambo kuonyesha hashindwi, alifunga mabao mengine matano kwa kichwa katika michezo dhidi ya Mtibwa Sugar (2-1) dk 31, Alliance (3-0) dk 18, Mbeya City (1-2) dk 41, Kagera (1-2) dk 20 na Ruvu Shooting (3-2) dk 90. Huku katika mguu wa kulia akifunga dhidi ya Biashara United (2-1).

Lakini wataalamu wa soka wanampa Kagere nafasi ya kuja kumfunika Makambo kwa staili za ufungaji wa mabao kwani bado ana mechi kadhaa za viporo mkononi na ameendelea kutisha na guu lake la kulia likionekana ndiyo mkombozi kwake zaidi ambapo mabao saba amefunga kutumia mguu huo.

Kagere amefunga kutumia mguu wa kulia mabao saba, sita akiwa ndani ya boksi na moja akiwa nje ya boksi. Amefunga ndani ya boksi dhidi ya Prisons (1-0) dk 2, Mwadui FC (3-1) dk50, Ruvu (0-5) dk 24, JKT (0-2) dk 12,38, Azam (1-3) dk 77 na nje ya boksi dhidi ya Lipuli FC(1-3) dk 58.

Kwenye vichwa hapa wamefungana na Makambo kila mmoja akifunga mabao matano. Amefunga dhidi ya Mbeya City (2-0) dk 11, 45, Mwadui FC (0-3) dk 50, Yanga (0-1) dk 71 na Azam (1-3) dk 4.

Na katika mabao 12 ambayo amefunga Kagere hakuna bao ambalo ametumia mguu wa kushoto ni kulia pamoja na vichwa tu.

Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA