TUUFYEKELEE MBALI UYANGA NA USIMBA TUWE NA NGUVU MOJA, VIPORO NA MAANDALIZI TFF MLITAZAME KWA UKARIBU
REKODI zimewekwa ili zivunjwe hivyo kwa sasa kuna suala jipya ambalo limeandikwa tena kwenye vitabu vya rekodi.
Miaka 39 ni mingi na inatoa picha kwamba kulikuwa kuna kitu ambacho awali hakikuwa sawa na sasa kimemalizika moja kwa moja.
Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania mnapaswa kupokea pongezi kwa kuonyesha Ushujaa mbele ya timu ngumu ambayo ilikuwa haifungiki.
Wakati mnaingia vitani nina amini milIkuwa mnatambua nini mnahitaji na mkaamua kuungana kwa pamoja kupambana kwa ajili ya Taifa hicho ndicho kinatakiwa.
Kwa hatua ambayo mmefikia mnapaswa mtambue kwamba ni mwanzo wa hatua nyingine ngumu zaidi ya mliyotoka hakuna muda wa kupumzika. Kama mtaendelea kufurahia ushindi mpaka kesho itakuwa ni rahisi kuanguka kutokana na namna ushindani ulivyo.
Kwa sasa baada ya kufuzu Afcon akili zenu na mawazo yenu nayo yanatakiwa kubadilika haraka ili kwenda sawa na upepo namna unavyokwenda kimataifa.
Kikubwa kinachohitajika kwenye mpira ni maandalizi mazuri na sahihi hali itakayosaidia kupatikana kwa matokeo chanya uwanjani hakuna uchawi mwingine hapo.
Hivyo wachezaji rekodi ambayo mmeivunja mnapaswa mpambane iwe ya muendelezo kwa sasa kutokana na mazingira kuwahukumu endapo mtabweteka.
Pia jambo jingine ambalo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linatakiwa lishtuke mapema ni hali halisi iliyopo kwenye mashindano ya kimataifa.
Matarajio ya mashindano haya hatua ya Makundi inatarajiwa kuanza mwezi Juni, mwezi ambao ukitazama kwa mujibu wa kalenda ya mashindano ligi itakuwa imekamilika.
Hapo ndipo huwa kuna kuwa na ugumu kidogo hasa kwa maandalizi ya wachezaji wetu pamoja na namna ya kuwafanya wawe ni bora muda wote.
Isitoshe kwa namna ratiba inavyokwenda usishangae ikatokea kwamba bado muda huo timu ya Simba itakuwa ina viporo mkononi hali ambayo itakuwa na ugumu kwa baadhi ya timu.
Kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni mipango makini ili kabla ya mwezi wa mashindano kufika tuwe tumekamilisha mipango yetu pamoja na ratiba kiujumla.
Kila kitu kinawezekana iwapo mipango itapangwa mapema na sio kusubiri muda wa mashindano ndipo tunaanza kukimbizana na wachezaji pamoja na viongozi hii sio sawa.
Wachezaji mnapaswa mtambue kwamba hatua ambayo mmefika kwa sasa ina ugumu wake ukizingatia mnakutana na timu bora na zenye uchu wa kupata matokeo.
Imani yangu ni kwamba kwa kuwa mliweza kufuzu basi na kutinga mpaka robo fainali inawezekana hata kufika fainali pia hakuna kisichowezekana.
Mtambue kwamba kwa kila hatua ambayo mnaipiga kwa sasa ni mafanikio kwa Taifa kwani viwango vya soka taratibu vinapanda hali inayopandisha ramani ya soka letu.
Kama ilivyokuwa kwa Simba namna ambavyo wametinga hatua ya robo fainali ndivyo itakavyokuwa na kwenu pia kufanya furaha iendelee kuwepo siku zote.
Ni muda wa kutazama namna itakayotutoa hapa tulipo na kufika mbele zaidi kwa kuangalia mapungufu ambayo tumeyafanya wakati uliopita.
Mashabiki pamoja na kamati ya hamasa wote mmefanikiwa kufikia malengo yenu kwani kamati ya hamasa imefanikiwa kuwafikia walengwa na walengwa nao wamejibu kwa kujitokeza uwanjani.
Kwa hamasa ambayo ilijitokeza uwanja wa Taifa inaonyesha ni namna gani watanzania wanapenda mpira hali inayowafanya wawe wazalendo hasa inapocheza timu yao ya Taifa.
Pia kitendo cha kuuvua ushabiki ule wa Usimba na Uyanga, kimeonesha namna tulivyokomaa hasa katika kuonyesha uzalendo.
Muendelezo uwe kwenye mechi zote, timu zipeane sapoti kila inapotakiwa bila kuonyesha chuki kwani sisi wote ni wamoja.
Tukiungana tutapata matokeo chanya kama ambavyo imetokea kwa timu yetu ya Taifa, mashabiki wa Yanga waiunge mkono Simba kwenye michuano ya kimataifa hata Simba pia mtatakiwa kuiunga mkono Yanga ikiwa kwenye majukumu ya kimataifa.
Chuki za mashabiki hazijengi bali zinabomoa na kufanya mpira wetu ubaki palepale ulipo tubadilike na tupeane sapoti kwa maendeleo yetu.
Comments
Post a Comment