MADAGASCAR YAIPIGA NIGERIA 2-0 NA KUFUZU 16 AFCON, UGANDA NAYO YAPETA

MADAGASCAR imeshitua baada ya kuichapa Nigeria 2-0 katika mchezo wa mwisho wa Kundi B Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 Jumapili Uwanja wa Alexandria nchini Misri.
Ushindi huo umetokana na mabao ya nyota wake, kiungo wa Paris ya Ligue 2 Ufaransa, Lalaina Nomenjanahary dakika ya 13 na mshambuliaji wa Ohod ya Saudi Arabia, Charles Carolus Andriamatsinoro dakika ya 53.
Kwa matokeo hayo, Madagascar imemaliza kileleni mwa Kundi B ikifikisha pointi saba kufuatia kushinda mechi mbili sare moja, ikifuatiwa na Nigeria iliyomaliza na pointi sita na zote zinasonga hatua ya 16 Bora.


Kiungo wa Madagascar, Lalaina Nomenjanahary akishangilia baada ya kufunga bao la kwanza

Guinea pamoja na kuifunga Burundi 2-0, mabao ya mshambuliaji wa Auxerre ya ya Ligue 2 Ufaransa, Mohamed Lamine Yattara dakika za 25 na 52 Uwanja wa Al Salam mjini Cairo, lakini imemaliza nafasi ya tatu kwa pointi zake nne. Burundi imeshika mkia baada ya kufungwa mechi zote tatu.
Nayo Uganda imefanikiwa kwenda hatua ya 16 Bora licha ya kuchapwa mabao 2-0 na wenyeji, Misri mabao ya mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah dakika ya 36 na kiungo wa Aston Villa, Ahmed El Mohamady dakika ya 45 na ushei katika mchezo wa Kundi A Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.
Uganda wamebebwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliyoichapa Zimbabwe 4-0, mabao ya mshambuliaji wa Antwerp ya Ubelgiji, Jonathan Bolingi dakika ya nne, mshambuliaji wa Beijing Guoan ya China, Cedric Bakambu dakika ya 34 na 65 na mshambuliaji wa Middlesbrough ya England, Britt Assombalonga dakika ya 78 Uwanja wa Juni 30 mjini Cairo.
Kwa matokeo hayo, Misri imemaliza kileleni mwa Kundi A kwa pointi zake tisa, ikifuatiwa na Uganda pointi nne, DRC pointi tatu na Zimbabwe pointi moja.
Michuano hiyo itaendelea Jumatatu kwa mechi za Kundi D Afrika Kusini na Morocco na Namibia na  Ivory Coast zote kuanzia Saa 1:00 usiku na za Kundi C, Kenya na Senegal na Tanzania na Algeria kuanzia Saa 4:00 usiku.
Kwa sasa Algeria inaongoza Kundi C kwa pointi zake sita, ikifuatiwa na Kenya yenye pointi tatu sawa na Senegal, wakati Tanzania inashika mkia haina pointi.
Kundi D Morocco inaongoza kwa pointi zake sita ikifuatiwa na Ivory Coast pointi tatu sawa na Afrika Kusini, wakati Namibia ambayo haina pointi inashika mkia.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA