SAMATTA AISAIDIA GENK KUANZA VYEMA KUTETEA TAJI LA LIGI YA UBELGIJI, YASHINDA 2-1

Na Mwandishi Wetu, GENK
MSHAMBULIAJI wa Kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku wa Ijumaa ameisaidia timu yake, KRC Genk kuanza vyema msimu mpya wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya KV Kortrijk.
Samatta alicheza kwa dakika zote 90 mechi hiyo ya Uwanja wa nyumbani, Luminus Arena mjini Genk, ingawa tu alikuwa chini ya ulinzi mkali wa mabeki wa KV Kortrijk na haikuwa ajabu alipomaliza bila kufunga.
Wageni walitangulia kwa bao la kiungo Julien De Sart dakika ya 14, kabla ya mshambuliaji Msweden Benjamin Nygren kuwasawazishia mabingwa watetezi, Genk dakika ya 50 na kiungo Mturuki, Ianis Hagi kufunga la ushindi dakika ya 76.
Mbwana Samatta ameisaidia KRC Genk kuanza vyema msimu mpya wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji 


Mbwana Samatta akiwania mpira wa juu dhidi ya kipa wa KV Kortrijk, Sebastien Bruzzese 

Samatta mwenye umri wa miaka 26, ameichezea Genk jumla ya mechi 157 za mashindano yote na kuifungia mabao 62 tangu amejiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Katika ligi ya Ubelgiji pekee amefunga mabao 47 katika mechi 123, kwenye Kombe la Ubelgiji amefunga mabao mawili katika mechi tisa, Super Cup mechi moja na Europa League amefunga mabao 14 katika mechi 24.
Kikosi cha KRC Genk kilikuwa: Vukovic, Uronen, Dewaest, Cuesta, Maehle, Berge, Heynen, Nygren/Hagi dk74, Benson/Paintsil dk64, Ito/Piotrowski dk89 na Samatta.
KV Kortrijk: Bruzzese, Golubovic, Hines-Ike, Kagelmacher, Mboyo/Ezekiel dk71, Kage/Ocansey dk54, Van Der Bruggen, Ajagun/Rolland dk67, De Sart, Batsula na D'Haene.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA