SIMBA SC WAENDA KAMBINI AFRIKA KUSINI, QUEENS NAO WAENDA UJERUMANI KUJIFUA

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM  
KIKOSI cha Simba SC kimeondoka leo Dar es Salaam kwenda Afrika Kusini kuweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya.
Mabingwa hao wa Tazania Bara wanaondoka baada ya kukamilisha usajili wa kikosi chake, ambacho msimu ujao wamekwenda Afrika Kusini kwa maandalizi ya msimu mpya. 
Wachezaji wote walikusanyika katika hoteli ya Sea Scape, eneo la Kunduchi mjini Dar es Salaam kwa maandalizi ya safari.
Na jana asubuhi ilifanyika Semina ya ndani ya wachezaji na benchi la ufundi kuhusu historia ya Simba, kanuni, maadili, desturi, nidhamu na malengo ya timu kwa msimu wa 2019/2020 katika hoteli ya Sea Scape.




Yote hayo yalitanguliwa na kikao cha odi ya Wakurugenzi Jumamosi kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Mohamed ‘Mo’ Dewji na kuhudhuriwa pia na Mwenyekiti wa klabu, Swedi Nkwabi wawili ambao inadaiwa wametofautiana.
Kuelekea msimu ujao, tayari Simba SC imesajili wachezaji 11 wapya hadi sasa, ambao ni kipa Beno David Kakolanya, baki Gardiel Michael Mbaga na kiungo Ibrahim Ajibu Migomba wote kutoka Yanga SC, ambao kwa pamoja na beki wa kati, Kennedy Wilson Juma kutoka Singida United na Miraj Athuma I ‘Madenge’ kutoka Lipuli wanafanya idadi ya wachezaji watano wazawa wapya Msimbazi hadi sasa.
Wengine sita wote ni wa kigeni, Wabrazil mabeki beki Gerson Fraga Vieira ATK ya Ligi Kuu ya India na Tairone Santos da Silva kutoka klabu ya Atletico Cearense FC, mshambuliaji, Wilker Henrique da Silva kutoka Bragantino, zote za Daraja la Nne nchini Brazil na viungo Mkenya, Francis Kahata Nyambura, Msudan Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman na winga Deo Kanda kutoka TP Mazembe ya kwao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Pamoja na kusaini wachezaji wapya, Simba SC pia imewapa mikataba mipya wachezaji wake kadhaa wa msimu uliopita, wakiwemo kipa Aishi Manula, mabeki Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Nahodha Msaidizi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala, Muivory Coast, Serge Wawa Pascal viungo Jonas Mkude, Mzambia Clatous Chama na washambuliaji Nahodha Mkuu, John Bocco na Meddie Kagere raia wa Rwanda.
Miongoni mwa wachezaji watakosekana Simba SC ni pamoja na Waganda, beki Juuko Murshid na mshambuliaji Emmanuel Okwi ambao wote wanaondoka.
Wakati huo huo: Mapema Alfajiri kikosi cha timu ya wanawake, Simba Queens kwenda nchini Ujerumani kwa ziara ya kisoka ya wiki mbili, chini ya mkuu wa msafara, Asha Baraka ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.
Wakiwa nchini humo, wachezaji wa Simba Queens watapata nafasi ya kushiriki semina mbalimbali za kijamii ambazo zina lengo la kuwapa mbinu mbadala za kazi ambazo wanaweza kufanya nje ya maisha ya soka.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA