MO DEWJI AWATULIZA WANA SIMBA SC BAADA YA KUTOLEWA MAPEMA LIGI YA MABINGWA

Na Saada Salim, DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Bodi ya Ukurugenzi ya Simba SC, Mohammed ‘Mo’ Dewji amewataka wapenzi na wanachama wa klabu hiyo kuwa wavumilivu baada ya timu kutolewa mapema katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afri 
Mabingwa wa Tanzania, Simba SC walitupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na UD Songo ya Msumbiji katika mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza Jumapili Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Na baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 mjini Beira wiki mbili zilizopita, maana yake Simba SC ilitolewa kwa sheria ya mabao ya ugenini.

Mohammed ‘Mo’ Dewji amewataka wana Simba SC wawe wavumilivu baada ya timu kutolewa mapema Ligi ya Mabingwa  

Baada ya kimya cha tangu Jumapili kufuatia kutolewa na UD Songo, Mo Dewji ameibuka leo kuwaomba msamaha wana Simba na kuahidi matokeo mazuri sehemu iliyobaki ya msimu.  
“Wanasimba, mnisamehe kwa ukimya. Maumivu ya matokeo yametupata sote. Naomba tukumbushane: Sisi ni SIMBA! Simba lazima anyanyuke! Hawezi kukata tamaa. Niwaombe tusivunjike moyo wala kukata tamaa. Hatutaogopa maneno ya watu na hatutaacha kupambana na kujipanga kwa ajili ya malengo yetu,”amesema.
Mo Dewji ambaye ni Mbunge wa zamani wa jimbo la Singida Mjini (CCM) amesema kwamba msimu huu watautumia kikamilifu kuhakikisha wanaboresha mipango yao ili msimu ujao warudishe furaha ya wapenzi wa klabu hiyo.
“Tumwombe Mwenyezi Mungu atutangulie katika safari yetu endelevu. Tukumbushane tena: Roma haikujengwa kwa siku moja. Tuwe wavumilivu, tutafika tu Insha’Allah,”alisema.
Baada ya kuitoa Simba SC, sasa UD Songo watamenyana na FC Platinum ya Zimbabwe iliyowatoa jirani zao, Big Bullets ya Malawi kwa mabao 3-2 ushindi wa ugenini Jumamosi kufuatia sare ya 0-0 nyumbani kwenye mchezo wa kwanza. 
Msimu uliopita Simba SC ilikuwa na bahati baada ya kufanikiwa kufika hadi Robo Fainali ambako ilitolewa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kufuatia kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi D, nyuma ya Al Ahly ya Misri, ikizipiku AS Vita ya DRC na JS Saoura ya Algeria.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA