KAGERE AENDELEZA MOTO WA MABAO SIMBA SC YAICHAPA BIASHARA UNITED 2-0 MUSOMA

Na Mwandishi Wetu, MUSOMA
MABINGWA watetezi, Simba SC wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuwachapa wenyej, Biashara United 2-0 jioni ya leo Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara.
Ushindi huo uliotokana na mabao ya washambuliaji wake hatari, Mnyarwanda Meddie Kagere na mzawa, Miraj Athumani ‘Madenge’ unaifanya Simba SC inayofundishwa na Mbelgiji, Patrick Aussems ifikishe pointi 12 baada ya kushinda mechi zake zote nne za mwanzo, mbili ugenini.
Kagere aliye katika msimu wake wa pili Msimbazi tangu awasili kutoka Gor Mahia ya Kenya alifunga bao lake la kwanza dakika ya 22 akimalizia kwa shuri la chini kros ya Miraji Madenge kutoka upande wa kulia.

Miraj Athumani anayefahamika pia kama Shevchenko ambaye amerejeshwa Msimbaz msimu huu baada ya kuachwa miaka minne iliyopita alifunga bao lake dakika ya 53 kwa kchwa akimalizia mpira wa adhabu wa Ibrahim Ajibu.
Kikosi cha Biashara United kilikuwa; Daniel Mgoke, Innocent Edwin, Victor Hangaya/Lambaka Jerome dk50, Mpapi Salum, Justine Bilal, Juma Mpakala, Ally Kombo/Ramadhani Chombo ‘Redondo’ dk74, Derick Mussa, Yassir Duku, Lenny Kissu na Abdulmajid Mangaro.
Simba SC; Aishi Manula, Haruna Shamte, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Said Ndemla, Hassan Dilunga, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu/Sharaf Eldn Shiboub dk76 na Miraj Athumani ‘Madenge’/Deo Kanda dk80. 
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Hassan Materema dakika ya 49 limeipa ushindi wa ugenini JKT Tanzana 1-0 dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar Uwanja wa Kataba mjini Bukoba.
Nao Mtibwa Sugar wakafikisha mechi tano za kucheza bila ushindi kufuatia sare ya 1-1 na Mbeya City jioni ya leo Uwanja wa Jamhuri. Mtibwa walitangulia kwa bao la kungo mkongwe, Abdulhalim Humud dakika ya 23, kabla ya Peter Mapunda kuisawazisha MCC dakika ya 43.
Na bao la dakika ya 52 la Salum Chubi likainusuru Ndanda SC kuzama mbele ya KMC iliyotangulia kwa bao la Ally Ramadhan dakika ya tisa, timu hizo zikitoka sare ya 1-1 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
Na Lipuli FC ikalazimishwa sare ya 2-2 na Tanzania Prisons Uwanja wa Samora mjini Iringa, mabao yake yakifungwa na David Kameta dakika ya 18 kwa penalti na Paul Materaz dakika ya 45, wakati ya wageni yamefungwa na Hamidu Daudi dakika ya sita na Cleophas Mkandala dakika ya 83.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA