SAMATTA APAMBANA HADI MWISHO KRC GENK YAPOKONYWA USHINDI MWISHONI UBELGIJI

Na Mwandishi Wetu, TRUIDEN 
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku huu amecheza kwa dakika zote 90 timu yake, KRC Genk ikitoa sare ya 3-3 na Sint-Truiden katika mchezo wa ugenini wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji usiku Uwanja wa Stayen.
KRC Genk ilikaribia kuondoka na ushindi mnono baada ya kuongoza kwa 3-0 hadi baada ya saa moja kwa mabao ya mshambuliaji mpya chipukizi, Mbelgiji Theo Bongonda Mbul'Ofeko Batombo dakika ya 15 akimalizia pasi ya kiungo Mromania mzaliwa wa Uturuki, Ianis Hagi aliyefunga mabao mengine mawli yote kwa penalti dakika za 48 na 60.

Lakini Sint-Truiden wakazinduka na kusawazisha mabao yote nusu saa ya mwisho, mshambuliaji Muivory Coast mzaliwa wa Ufaransa, Yohan Boli akifunga mawli dakika ya 63 na 87 na lingine beki Mspaniola Pol Garcia dakika ya 80.
Matokeo hayo yanawaacha Genk, mabingwa watetezi nafasi ya sita wakiwa na ponti 14 baada ya kucheza mechi tisa, wakizidiwa pointi sita na vinara, Club Brugge wenye pointi 20 za mechi nane, wakifuatiwa na Standard Liege pointi 18 za mechi nane, Gent pointi 17 za mech nane, Royal Excel Mouscron pointi 16 za mechi tisa na Royal Antwerp pointi 15 za mechi saba.
Kwa Samatta mwenye umri wa miaka 26 leo amecheza mechi ya 165 kwenye mashindano yote tangu ajiunge na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa amefunga mabao 68 jumla.
Katika ligi ya Ubelgiji pekee amecheza mechi 130 na kufunga mabao 52, kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili, katika Super Cup mechi moja, Europa League mechi 24, mabao 14 na Ligi ya Mabingwa mechi moja, bao moja.
Kikosi cha Sint-Truiden kilikuwa; Schmidt, Garcia, Botaka, Sankhon, Boli, De Bruyn/Ito dk62, De Ridder, Mmaee, Janssens/Suzuki dk43, De Smet na Acolatse/Sousa dk71.
KRC Genk: Coucke, Mæhle, Dewaest, Lucumí, Uronen, Berge, Hrosovsky, Hagi/Heynen dk68, Ito, Bongonda/Paintsil dk67 na Samatta.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA