THOMAS ULIMWENGU ASAINI MKATABA WA MIAKA MIWILI KUREJEA KLABU YA TP MAZEMBE

Na Mwandshi Wetu, LUBUMBASHI
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga tena na klabu yake, TP Mazembe.
Ulimwengu mwenye umri wa miaka 27, amerejea Kamalondo ambako aliondoka mwaka 2016 kwenda Ulaya, ambako hata hivyo hakufanikiwa. 
Kati ya mwaka 2017 na 2018 alichezea na klabu za AFC Eskilstuna ya Sweden na FK Sloboda Tuzla ya Bosnia kabla ya kurejea Afrika na kuchezea klabu za Al Hilal ya Sudan na JS Saoura ya Algeria.
Na sasa amejiunga tena na Mazembe kama mchezaji huru na anatarajiwa kuwasil Lubumbashi Jumatano kuanza tena maisha mapya katika mji aliouzoea.
Ulimwengu anafanya idadi ya Watanzania katika klabu hiyo kufika watatu, baada ya kiungo Ramadhani Singano ‘Messi’ na mshambulaji Eliud Ambokile.
Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United.
Alicheza Moro United kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya AFC Eskilstuna ya Sweden, alikocheza hadi mwaka 2011  alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.
Ulimwengu alihamia Ulaya baada ya kushinda mataji makubwa akiwa na Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA