DK MSOLLA AWASIMAMISHA ‘WABISHI’ WAWILI KATIKA ORODHA YA WAPINGA UDHAMINI WA GSM

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
UONGOZI wa Yanga SC umewasimamisha wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji, Salim Rupia na Frank Kamugisha kuanzia leo Machi 27, 2020 hadi hapo mkutano mkuu utakapofanya maamuzi kwa mujibu wa katiba.
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa klabu, Dkt. Mbette Mshindo Msolla leo, imesema kwamba uamuzi huo umefikiwa leo baada ya kikao cha siku mbili mfululizo kilichofanyika Dar es Salaam kuanzia Mach 26 hadi 27.
Na hatua hiyo imefuatia kutokea sintofahamu iliyosababisha mdhamini wa klabu, Kampuni ya GSM kusitisha kutoa misaada iliyo nje ya mkataba wake.
Aidha, Kamati ya Utendaji ya Yanga imepokea na kukubali maombi ya wajumbe wengine watatu, Rodgers Gumbo, Shijja Richard na Said Kambi kujiuzulu nafasi zao na kwamba nafasi ya mjumbe wa kuchaguliwa itajazwa mara moja kwa mujibu wa Ibara ya 29(3) wa Katiba ya Yanga.
Wakati huo huo Kamati ya Utendaji wa Yanga imewasilisha barua GSM kujibu barua yao yenye kumbu kumbu namba GSMGROUP/YANGA/LETTER/2/2020 ya tarehe 24/03/2020 kuhusu kujitoa udhamini wa maswala yasiyo ya kimkataba. 
Taarifa ya Mwenyekiti, Dk. Msolla imesema kwamba Barua hiyo imewasilishwa baada ya maamuzi ya pamoja ya kikao cha Kamati ya Utendaji leo.
Shijja na Kambi walikuwa Wajumbe wa kuteuliwa wakati Rupia, Kamugisha na Gumbo ni miongoni mwa Wajumbe waliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Mei 5, mwaka jana Jijin Dar es Salaam.
Sasa Kamati ya Utendaji Yanga inabaki na Wajumbe watano wa kuchaguliwa ambao ni Hamad Islam, Mhandisi Bahati Faison Mwaseba, Dominick Ikute, Arafat Haji na Saad Khimji pamoja na Dk. Athumani Kihamia pekee wa kuteulwa chini ya Mwenyekiti Dk. Msolla na Makamu Mwenyekiti, Frederick Mwakalebela.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA