RAIS MKAPA ALIYEWAPA WATANZANIA ZAWADI YA UWANJA WA KISASA WA MICHEZO AFARIKI DUNIA

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
RAIS mstaafu wa Serikali ya awamu ya tatu nchini, Benjamin William Mkapa aliyefanikisha ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa michezo Tanzania (Uwanja wa Taifa) uliopo Dar es Salaam amefariki dunia usiku wa kuamkia leo.
Taarifa ya kifo cha Mzee Mkapa imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli usiku wa kuamkia leo kupitia Televisheni ya Taifa, TBC.
Rais Magufuli amesema kwamba kiongozi huyo wa zamani wa taifa amefariki katika hospitali moja jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu.
“Mzee Benjamin William Mkapa Rais wa awamu ya tatu amefariki. Amefariki kwenye hospitali mjini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa. Niwaombe watanzania tulipokee hili. Taifa limepata msiba mkubwa. Tuendelee kumuombea Mzee wetu Rais Benjamin William Mkapa ambaye ametangulia mbele ya haki," amesema Rais Magufuli.
Katika ukurasa wake rasmi wa mtandao wa Twitter rais Magufuli amemuomboleza Mkapa na kusema atamkumbuka "kwa mapenzi yake makubwa kwa Taifa, ucha Mungu, uchapakazi na utendaji wake katika kujenga uchumi."
Mzee Mkapa alizaliwa Novemba 12 mwaka 1938, kijiji cha Ndanda, jirani na Masasi mkoani Mtwara na alikuwa Rais wa kwanza wa Tanzania baada ya demokrasia ya Vyama Vingi vya siasa kuanzia mwaka 1995 hadi 2005.
Wanamichezo nchini watamkumbuka daima Mzee Mkapa kutokana na kuwaachia Uwanja mzuri wa kisasa wa michezo – Taifa uliopo Dar es Salaam.
Wakati anafunga Michezo ya UMISETA mwaka 2000, Rais Mkapa alitoa ahadi ya kuwaachia watanzania Uwanja mzuri wa kisasa michezo kabla ya kumalza muda wake mwaka 2005 – lakini ulifunguliwa mwaka 2007.   Mungu ampumzishe kwa amani Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Ben Mkapa.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA