IBRAH CLASS ATWAA TAJI LA WBF BAADA YA KUMDUNDA MMALAWI

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
BONDIA Ibrahim Mgendera ‘Ibrah Class’ amefanikiwa kutwaa taji la WBF Intercontinental uzito wa  Super Light baada ya kumshinda Dennis Mwale wa Malawi kwa poonti za majaji wote katika pambano la raundi la 12 usiku wa jana ukumbi wa Next Door Arena, Masaki Jijini Dar es Salaam.
Class jana ameshinda pambano la 26 tangu aanze ngumi za kulipwa Juni 26 mwaka 2010, kati ya hayo 11 ameshinda kwa KO, wakati mengine sita amepigwa, matatu kwa TKO. 
Mgeni rasmi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa alikuwepo ukumbini jana na akamvisha Ibrah Class taji hilo jipya ambalo linafanya awe na mikanda minne jumla, mengine WPBF, GBC na AAC (All Africans Champion). 


Class amepigwa na Mtanzania mwenzake mmoja tu, Said Zungu Julai 26, mwaka 2010 ukumbi wa Swai Garden Pub Jijini Dar es Salaam katika pambano lake la kwanza kabisa na baada ya hapo, wengine waliomshinda ni wageni tu na tena wakiwa nyumbani kwao.
Watanzania wengine wawili waling’ara pia, Shaaban Jongo alimpiga Mmarekani Shawn Michael Miller kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya kwanza uzito wa Heavy na kutwaa taji la WBF International, wakati Nassib Ramadhani alimshinda kwa Knockout (KO) raundi ya pili Nkosinathi Biyana wa Afrika Kusini uzito wa uzito wa Feather.
Watanzania wengine watatu walichapwa, Imani Daudi Kawaya alishindwa kwa pointi na Ardi Ndembo wa Kongo uziro wa Heavy na mabinti Happy Daudi Mwaijike amedundwa kwa KO raundi ya pili na Lolita Muzeya wa Zambia uzito wa Super-Welter na Stumai Muki ameshindwa kwa pointi na Revai Madondo wa Zimbabwe uzito wa Light.
Vijana wa nyumbani pia walichapana baina  yao katika mapambano mengine mawili, Hafidh David akampiga kwa TKO Kaminja Ramadhan raundi ya kwanza na uzito wa Cruiser na Hashim Japhari Kiranga akamshinda Said Mlosi Mussa kwa pointi uzito wa Light. 
Naye Tervel Pulev wa Bulgaria, mdogo wa Kubrat alikuwa ana usiku mzuri katika ardhi ya Dar es Salaam baada ya kumshinda Vikapita Merero wa Namibia kwa TKO raundi ya tisa uzito wa Cruiser pia.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA