WAZIRI MKUU MGENI RASMI TAMASHA LA UTAMADUNI
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi kwenye Tamasha la kwanza la kihistoria la Utamaduni kitaifa Julai 2, 2022 Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania aliyoyatoa kwenye Tamasha la Utamaduni la Mkoa wa Kilimanjaro la kutaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuandaa tamasha kubwa la kitaifa la utamaduni litakaloshirikisha mikoa yote ya Tanzania ili kutangaza hazina ya utamaduni wa makabila ya Tanzania Duniani.
Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amefafanua kuwa tamasha hilo litaambatana na matembezi maalum ya kitamaduni (Utamaduni Carnival) katika jiji la Dar es Salaam ambayo yameandaliwa njia maalum za kupita ikiwemo daraja la juu la Mfugale, Kijazi, Tanzanite na daraja la mwalimu Nyerere.
Amesema, tamasha hilo litatoa fursa kwa makabila yote nchini kuonesha tamaduni zao kupitia ngoma na vyakula vya asili ili kukuza utalii wa kiutamaduni.
Aidha, amewataka watanzania kujitokeza kushiriki kwenye tamasha hilo la kwanza la kitaifa ambalo licha ya kutoa burudani, litaonesha vitu muhimu vya kiutamaduni na kutoa fursa kwa wageni kujifunza.
Ameongeza kuwa, tamasha hilo litakuwa la siku tatu ambapo siku inayofuata ya Julai 3, 2022 itakuwa na tukio maalum la mirindimo ya taarabu ambapo limeainishwa kama usiku wa taarabu utakaofanyika eneo la ufukwe wa Coco Beach maarufu kwa wachoma mihogo kuanzia saa 8:00 hadi saa 6:00 usiku.
Amesema shamrashamra hizo zitashamirishwa na vikundi mbalimbali vya wasanii kutoka ndani na nje ya Tanzania kama Comoro, Burundi na Kenya, pia wasanii wa taarabu nchini akiwemo Mzee Yusufu, Hadija Kopa, Patricia Hillay, Abuduli Misambano na Aisha Mashauzi watakuwepo kutumbuiza usiku huo.
Comments
Post a Comment