IHEFU YAZIMA REKODI YA YANGA KUTOFUNGWA MECHI YA 50


WENYEJI, Ihefu SC wamezima wimbi la Yanga kutopoteza mechi katika mchezo wa 50 baada ya ushindi wa 2-1 leo Uwanja wa Highland Estate huko Mbarali mkoani Mbeya.
Haukuwa ushindi mwepesi, kwani ilibidi Ihefu watoke nyuma baada ya Yanga kutangulia na bao la Mchezaji Bora wa Ligi Kuu, kiungo Mkongo Yanick Bangala Litombo dakika ya tisa.
Kiungo Mzimbabwe, Never Tigere aliifungia Ihefu SC bao la kusawazisha dakika ya 39, kabla ya Lenny Kissu kufunga la ushindi dakika ya 62.
Kwa ushindi huo wa pili tu wa msimu kwa Ihefu iliyorejea Ligi Kuu baada ya msimu mmoja tangu ishuke, inafikisha pointi 11 katika mchezo wa 14 na kusogea nafasi ya 13 kwenye ligi ya timu 16.
Yanga pamoja na kupoteza mchezo huo inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 32 za mechi 13 sasa, ikiizidi wastani wa mabao tu Azam FC ambayo pia imecheza mechi moja zaidi.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA