TANESCO YAJISAFISHA TATIZO LA TAA UWANJA WA MKAPA
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetolea ufafanuzi tatizo la taa wakati wa mchezo wa marudiano wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Yanga na Rivers United ya Nigeria leo Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam. Taa zilififia dakika ya 27 kabla ya kuzimika kabisa wakati wa mchezo huo na kulazimisha timu kurejea vyumbani kwa takriban dakika 20 na zilipowaka vikosi vikarejea kumalizia mechi. Yanga SC imefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika licha ya sare ya bila kufungana na Rivers United wakinufaika ushindi wa 2-0 ugenini kwenye mchezo wa kwanza Jumapili iliyopita Nigeria, mabao ya mshambuliaji Mkongo, Fiston Kalala Mayele. Yanga sasa itamenyana na Marumo Gallants ya Afrika Kusini ambayo imeitoa Pyramids ya Misri kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Cairo wiki iliyopita na kushinda 1-0 leo Phokeng, NW. Mechi ya kwanza Yanga na Marumo Gallants itafanyika Dar es Salaam Mei 10 na marudiano yatafuatia Afrika Kusini Mei 17.