YANGA FAIDA TUPU 2022-2023 KUJENGA UWANJA WA KISASA JANGWANI
KLABU ya Yanga msimu wa 2022-2023 imeingiza jumla ya Sh. Bilioni 17.8 kutokana na mapato mbalimbali, ikiwemo udhamini wao kutoka makampuni ya SportPesa, Azam Media Limited, Haier, GSM Group, Jembe Energy, CRDB Bank, Unicef, Smile na Robbialac.
Hayo yamesemwa na Rais wa Yanga, Mhandishi Hersi Ally Said katika Mkutano Mkuu wa mwaka klabu uliofanyika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Hersi amesema katika fedha hizo, matumzi ya klabu yamemuwa Bilioni 17.3, maana yake Faida ambayo wamevuna kutokana na wadhamini ni Sh. Milioni 500.
Aidha, Rais Hersi amesema msimu wa 2022-2023 klabu pia imevuna kiasi cha Bilioni 3.5 kutokana na zawadi za ushiriki wao kwenye mashindano mbalimbali na kwamba kwa msimu ujao Bajeti yao ya matumizi itakuwa zaidi ya Sh. Bilioni 20.
Pamoja na kutwaa Ngao ya Jamii, ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), Yanga ilishika nafasi ya pili Kombe la Shirikisho Afrika.
Rais Hersi amesema uongozi wake umedhamiria kujenga wa kisasa katika makao makuu ya klabu, Jangwani ambao utakuwa na uwezo wa kuingiza watu 15,000 hadi 18,000.
"Katika uongozi wangu, mimi na wenzangu hatutamaliza muda wetu mpaka tumalize ujenzi huu wa Uwanja," amesema Rais Hersi.
Katika Mkutano huo wametambulishwa Wajumbe wapya wa Baraza la Wadhamini wa Yanga wakiongozwa na mjane wa Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa kwanza wa Bara la Mapinduzi, marehemu Abeid Amaan Karume, Mama Fatma Karume.
Wajumbe wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Newala, Kapteni Mstaafu George Mkuchika, Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Iramba Magharibi, Dk Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Kinondoni, Tarimba Abbas na Naibu Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde.
Comments
Post a Comment