MAWAZIRI WA MICHEZO AFRIKA MASHARIKI WAJADILI UENYEJI AFCON 2027
MAWAZIRI wanaoshughulikia michezo katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda wamekutana kujadili maombi yao ya pamoja ya kuwa wenyeji wa Mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2027 kabla ya kwenda kuwasilisha maombi hayo ambayo yatapigiwa kura Septemba 27, 2023 Jijini Cairo Misri.
Kikao hicho kimefanyika leo Septemba 22, 2023 Jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti Mhe.Dkt. Damas Ndumbaro Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania ambapo Kenya imewakilishwa na Bw. Peter Kiplagat Tum ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Michezo nchini na Uganda imewakilishwa na Bw. Tashobya Ambrose ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo la nchi hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema nchi hizo zina nafasi kubwa na uwezo mkubwa wa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kwa kuwa zina Jiografia inayofanana na miundombinu ya michezo inayokidhi mashindano hayo pamoja na Serikali zote tatu kuwa tayari kukarabati miondombinu itakayotumiwa kwenye michezo hiyo.
Awali, akiwasilisha taarifa ya kikao Cha makatibu Wakuu kilichofanyika Septemba 21, 2023 Katibu Mkuu Bw. Yakubu amesema tayari nchi hizo kwa asilimia kubwa zinakidhi vigezo vilivyoanishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na wao kama nchi wameaanisha sababu mbalimbali za kutaka kuendesha mashindano hayo ikiwemo kuandaa makala itakayotoa ushawishi kwa wapiga kura kuonesha mwamko wa mchezo wa soka na utayari wa nchi hizo pia kupitia uhusiano wa kidiplomasia uliopo miongoni mwa nchi hizo.
Nchi nyingine inayowania wenyeji wa mashindano hayo ni Senegal na Botswana baada ya Nigeria kujitoa katika kinyang'anyiro hicho.
Comments
Post a Comment