NI MESSI TENA MSHINDI WA BALLON D'OR 2023, HAALAND NA MBAPPE...
GWIJI wa Argentina, Lionel Andrés Messi wa Inter Miami usiku wa jana amefanikiwa kushinda tuzo yake ya nane ya Ballon d'Or akiwaangusha Erling Haaland wa Manchester City na Kylian Mbappe wa Paris Saint-Germain.
Katika sherehe zilizofanyika ukumbi wa Theatre du Chatelet Jijini Paris – Messi, ambaye ni mshindi pia wa Ballon d’Or za mwaka 2009, 2010, 2011, 2012, 2015, 2019 na 2021 – jana alikabidhiwa tuzo hiyo na mmiliki mwenza wa klabu yake, Inter Miami, David Beckham.
Messi alifunga mabao mawili katika sare yab 3-3 na Ufaransa kabla ya Argentina kutwaa Kombe la Dunia kwa ushindi wa penalty 4-2 nchini Qatar mwaka 2022, likiwa taji la kwanza kwa nchi hiyo tangu 1986.
Kwa upande wake, kiungo wa Kimataifa Hispania, Aitana Bonmatí Conca anayechezea klabu ya Barcelona amefanikiwa kushinda tuzo ya Ballon d’Or upande wa wanawake, akiwashinda Sam Kerr wa Australia na klabu ya Chelsea na Mspaniola mwenzake, Salma Paralluelo wanayecheza naye Barcelona.
Tuzo ya Kopa Trophy imekwenda kwa Jude Bellingham wa England na Borrussia Dortmund akiwashinda Jamal Musiala wa Ujerumani na Bayern Munich na Pedri wa Hispania na Barcelona.
Tuzo ya Gerd Müller imechukuliwa na mshambuliaji wa Kimataifa wa Norway, Erling Braut Haaland wa Manchester City aliyefunga mabao 56 msimu uliopita na Tuzo ya Sócrates imekwenda kwa mshambuliaji wa Kimataifa wa Brazil, Vinícius Júnior anayechezea Real Madrid ya Hispania.
Tuzo ya Yashin Trophy imechukuliwa na kipa wa Kimataifa wa Argentina, Emiliano Martínez wa Aston Villa ambaye amewapiku Mbrazil, Ederson wa Manchester City na Yassine Bounou wa Morocco na Sevilla, huku Manchester City ikishinda Tuzo ya Klabu Bora kwa kuingiza wachezaji wengi Zaidi kwenye Fainali za Ballon d’Or.
Comments
Post a Comment