NYOTA MPYA AING’ARISHA TAIFA STARS UFUNGUZI KUFUZU KOMBE LA DUNIA
TANZANIA imeanza vyema harakati za kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Níger katika mchezo wa Kundi E leo Uwanja wa Marrakech mjini Marrakech nchini Morocco.
Akiichezea kwa mara ya kwanza Taifa Stars, kiungo mshambuliaji Charles William M'Mombwa mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ndiye aliyeifungia timu hiyo bao hilo pekee.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 anayecheza ya Macarthur FC ya Ligi Kuu ya Australia alifunga bao hilo dakika ya 56 Nahodha na mshambuliaji wa PAOK Thessaloniki FC ya Ugiriki, Mbwana Ally Samatta.
Mara tu baada ya mchezo huo, Taifa Stars inafunga safari kurejea nyumbani kwa ajili ya mechi ya pili ya Kundi E dhidi ya Morocco Jumanne Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam kuwania tiketi ya Fainali hizo zinazoandaliwa kwa pamoja na nchi za Canada, Mexico na Marekani.
Pamoja na Taifa Stars, Niger na Morocco timu nyingine zilizopo Kundi E ni Kongo na Zambia, wakati Eritrea imejitoa.
Timu tisa zitakazoongoza makundi zitafuzu moja kwa moja kuiwakilisha kwenye Fainali za Kombe la Dunia, wakati washindi wa pili bora wanne wa makundi watamenyana katika Nusu Fainali na Fainali na mshindi atakwenda kushiriki mchujo wa Mabara kuwania nafasi ya kwenda Kombe la Dunia pia.
Mchujo wa Mabara, unaojulikana kama Inter-Confederation Play-Offs ni michuano mingine midogo inayoshirikisha timu sita za Mabara manne duniani, kasoro UEFA pamoja na nchi mwenyeji kutoka CONCACAF kutafuta timu mbili za mwisho za kushiriki michuano hiyo.
Comments
Post a Comment