BURKINA FASO NA CAMEROON ZASONGA MBELE, ALGERIA WATOLEWA


TIMU ya Burkina Faso imefuzu Hatua ya Mtoano Fainali za Kombe la  Mataifa ya Afrika licha ya kuchapwa mabao 2-0 na Angola usiku wa jana katika mchezo wa mwisho wa Kundi D Uwanja wa Charles Konan Banny de Yamoussoukro mjini Yamoussoukro, Ivory Coast.
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki alicheza kwa dakika 89, kabla ya kumpisha Boureima Hassane Bandé wa HJK Helsinki ya Finland, mabao ya Angola yakifungwa na Mabululu dakika ya 36 na Zine dakika ya 90 na ushei.
Mechi nyingine ya Kundi D jana, bao pekee la beki wa Al Hudod ya Iraq, Mohamed Dellahi Yali dakika ya 37 liliipa Mauritania ushindi wa 1-0 dhidi ya Algeria Uwanja wa de Bouaké mjini Bouaké, Ivory Coast.
Angola imemaliza kileleni na pointi zake saba, ikifuatiwa na Burkina Faso pointi nne, wakati Mauritania nafasi ya tatu pointi tatu na Algeria iliyoambulia pointi mbili imeshika mkia.
Katika mechi za Kundi C zilizotangulia jana, mabingwa watetezi, Senegal walikamilisha mechi zao zote za makundi kwa ushindi baada ya kuilaza Guinea mabao 2-0 Uwanja wa Charles Konan Banny de mjini Yamoussoukro.
Mabao ya Senegal jana yalifungwa na beki wa Maccabi Haifa ya Israel, Abdoulaye Seck dakika ya 61 na mshambuliaji wa Marseille ya Ufaransa, Iliman Cheikh Baroy Ndiaye dakika ya 90 na ushei.
Lakini habari kubwa zaidi ni Cameroon kufuzu kufuatia ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Gambia Uwanja wa Bouaké.
Haukuwa ushindi mwepesi kwa Cameroon, kwani walilazimika kutoka nyuma baada ya Gambia kuongoza 2-1 hadi dakika ya 85.
Mabao ya Cameroon yalifungwa na washambuliaji Karl Toko-Ekambi wa Abha ya Saudi Arabia dakika ya 57, beki James Gomez wa Sparta Praha II ya Jamhuri ya Czech aliyejifunga dakika ya 82 na Christopher Wooh wa Rennes ya Ufaransa dakika ya 99 na ushei,
Kwa upande wao  Gambia mabao yao yalifungwa na kiungo wa Metz ya Ufaransa, Abdoulie Jallow dakika ya 72 na mshambuliaji wa Young Boys ya Uswisi, Ebrima Colley dakika ya 85.
Senegal imeongoza Kundi C kwa pointi zake tisa, ikifuatiwa na Cameroon pointi nne, ikiizidi tu wastani wa mabao Guinea, wakati Gambia imeshika mkia baada ya kufungwa mechi zote tatu.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA