MAN UNITED YAINYUKA LIVERPOOL 4-3 NA KUTINGA NUSU FAINALI KOMBE LA FA


WENYEJI, Manchester United wamefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Kombe la FA England baada ya ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Liverpool leo Uwanja wa Old Trafford Jijini Manchester.
Ilikuwa mechi ya funga nikufunge ndani ya dakika 120, ambayo mwishowe shujaa ameibuka mshambuliaji kijana mdogo wa miaka 21, Muivory Coast, Amad Diallo Traoré aliyefunga bao la ushindi dakika ya 120.
Katika dakika 90 timu hizo zilifungana mabao 2-2, kiungo Mscotland Scott Francis McTominay akianza que kuifungia Manchester United dakika ya 10, kabla ya kutoka nyuma kwa mabao ya kiungo Muargentina, Alexis Mac Allister dakika ya 44 na Mohamed Salah dakika ya 45'+2.
Mshambuliaji Mbrazil, Antony Matheus dos Santos akaisawazishia Manchester United dakika ya 87 baada ya 71 kuchukua nafasi ya Mdenmark, Rasmus Winther Højlund.
Mchezo ukaenda kwenye dakika 30 za nyongeza na Liverpool wakatangulia kwa bao la kiungo chipukizi wa Kimataifa wa England, Harvey Elliott dakika ya 105 na mshambuliaji Kimataifa wa England, Marcus Rashford kuisawazishia Manchester United dakika ya 112.
Wakati refa John Brooks anajitayarisha kuuhamishia mchezo kwenye mikwaju ya penalti kuamua mshindi - ndipo Diallo aliyetokea benchi dakika ya 85 kuchukua nafasi ya beki Mfaransa, Raphaël Varane akawapa Mashetani Wekundu tiketi ya Nusu Fainali dakika ya mwisho.
Diallo akatolewa kwa kadi nyekundu baada ya kufunga bao hilo kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kushangilia akiwa amevua jezi yake ambayo ni makosa.
Timu nyingine zilizotinga Nusu Fainali ni Chelsea ambayo imeitoa Leicester City kwa kuichapa 4-2, Manchester City iliyoitoa Newcastle United kwa kuichapa 2-0 na Coventry City iliyoitoa Wolverhampton Wanderers kwa kuichapa 3-2.
Katika Nusu Fainali Manchester United watakutana na Coventry City Aprili 20 na Manchester City dhidi ya Chelsea Aprili 21 Uwanja wa Wembley Jijini London.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA