NI AL AHLY NA ESPERANCE FAINALI LIGI YA MABINGWA AFRIKA
MABINGWA watetezi, Al Ahly wamefanikiwa kwenda Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) usiku wa jana Uwanja wa Cairo International Jijini Cairo.
Mabao ya Al Ahly jana yalifungwa na Mohamed Abdelmonem dakika ya 68, Wessam Haissam Abou Ali dakika ya 83 na Akram Tawfik dakika ya 90'+12 na kwa ushindi huo mnono wa nyumbani wanakwenda Faniali baada ya kulazimisha sare ya bila mabao kwenye mechi ya kwanza Lubumbashi.
Al Ahly itakutana na Espérance Sportive de Tunis ambayo jana nayo iliitoa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa kuichapa 1-0, bao pekee la beki Raed Bouchniba dakika ya 57 akimalizia pasi ya mshambuliaji Mbrazil, Rodrigo Rodrigues Uwanja wa Loftus Versfeld Jijini Pretoria.
Espérance inakwenda Fainali kwa ushindi wa jumla wa 2-0 kufuatia kushinda 1-0 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita bao la mshambuliaji mwingine Mbrazil, Yan Medeiros Sasse dakika ya 41 Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi Jijini Radès.
Katika Fainali, Esperance wataanzia nyumbani Jumamosi ya Mei 18 Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi Jijini Radès., kabla ya timu hizo kurudiana Mei Jumamosi ya Mei 25 Uwanja wa CairoInternational Jijini Cairo.
Comments
Post a Comment