YANGA YAICHAPA SIMBA SC 2-1 NA KUZIDI KUUKARIBIA UBINGWA MWINGINE LIGI KUU


MABINGWA watetezi, Yanga SC wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi watani wao, Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni hii Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 58 katika mchezo wa 22 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi saba zaidi ya Azam FC inayofuatia ikiwa pia imecheza mechi moja zaidi, wakati Simba SC inabaki na pointi zake 46 za mechi 21 nafasi ya tatu.  
Ilikuwa siku nzuri kwa wanasoka kutoka Afrika Magharibi, washambuliaji Joseph Guédé Gnadou (29) na Freddy Michael Kouablan (25) wote kutoka Ivory Coast na kiungo Stephane Aziz Ki (28) kutoka Burkina Faso waliofunga mabao kwenye mechi hiyo ya mahasimu wa Tanzania.
Aziz Ki alianza kuifungia Yanga dakika ya 20 kwa mkwaju wa penalti uliotolewa na refa Ahmed Arajiga wa Manyara kufuatia Mburkinabe huyo kuangushwa kwenye boksi na beki mzawa Hussein Kazi ambaye aliingia dakika ya 11 kuchukua nafasi ya beki Mkongo, Henock Inoga Baka aliyeumia.
Guede akaifungia Yanga bao la pili dakika ya 38 baada ya kuwazidi maarifa mabeki wa Simba kufuatia pasi ndefu ya kiungo Mganda, Khalid Aucho na kwenda kumlamba chenga kipa Mmoroco, Ayoub Lakred kisha kuumkwamisha mpira nyavuni.
Kipindi cha pili kocha wa Simba, Abdelhak Benchika alibadili mbinu na kumuingiza kiungo wa Kimataifa wa Msumbiji, Luis Jose Miquissone na Koublan kuchukua nafasi za viungo, Mkongo Fabrice Luamba Ngomana Mrundi Saido Ntibanzokiza ambao walikwenda kuongeza nguvu ya kushambulia.
Ilikuwa tofauti na mabadiliko yaliyofanywa na kocha Muargentina wa Yanga, Miguel Angel Gamondi aliyeanza kwa kuwatoa beki Muivory Coast, Kouassi Attohoula Yao na mshambuliaji Clement Mzize na kuwaingiza beki Bakari Mwamnyeto na mshambuliaji Mzambia, Kennedy Musonda ambao hawakuwa na madhara kwa wapinzani.
Koublan akaifungia bao la kufutia machozi dakika ya 74 baada ya kupokea pasi nzuri ya kiungo Mzambia Clatous Chotta Chama na kuwatoka vizuri mabeki wa Yanga kabla ya kumchambua kipa Djigui Diarrab raia wa Mali.
Baada ya bao hilo, Yanga wakaongeza nguvu kwenye kujilinda zaidi huku wakishambulia kwa kushitukiza, wakati Simba iliongeza kasi ya kushambulia kujaribu kusawazisha bao bila mafanikio.
Kikosi cha Yanga kilikuwa; Djigui Diarra, Kouassi Attohoula Yao/Bakari Mwamnyeto dk65, Joyce Lomalisa/Nickson Kibabage dk6, Ibrahim Hamad 'Bacca', Dickson Job, Maxi Mpia Nzengeli/Augustine Okrah dk85, Mudathir Yahya/Jonas Mkude dk85, Joseph Guede, Stephane Aziz Ki na Clement Mzize/Kennedy Musonda dk65.
Simba SC; Ayoub Lakred, Israel Mwenda, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Che Fondoh Malone Junior, Hennock Inonga/Hussein Kazi dk11, Babacar Sarr/Muzamil Yassin dk74, Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma/Freddy Michael dk58, Kibu Dennis, Saido Ntibanzokiza/Luis Miqquissone dk58 na Clatous Chama/Pa Omar Jobe dk74.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA