AZAM FC YAIPIKU SIMBA LİGİ YA MABINGWA, AZİZ Kİ MFUNGAJI BORA


MSIMU wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara umehitimishwa leo kwa Azam FC kumaliza nafasi ya pili nyuma ya mabingwa, Yanga huku vigogo, Simba SC wakimaliza nafasi ya tatu na Coastal Union nafasi ya nne.
Azam FC imemaliza nafasi ya pili baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya JKT Tanzania mabao ya Yeisson Fuentes Mandoza dakika ya 58 na Feisal Salum Abdallah dakika ya 71 Uwanja wa Sekondari ya Nyankumbu, Geita.
Simba imemaliza ilipokuwa, nafasi ya tatu licha ya ushindi wa 2-0 pia dhidi ya JKT Tanzania, mabao ya Saido Ntibanzokiza dakika ya 88 kwa penaltı Ande Essomba Onana dakika ya 90’+2 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Azam imemaliza na pointi 69, ikiizidi tu wastani wa mabao Simba SC - wote wakiwa nyuma ya Yanga iliyomaliza na pointi 80 baada ya ushindi wa 4-1 dhidi ya Tanzania Prisons leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga leo yamefungwa na Mburkinabe, Stephane Aziz Ki dakika ya 11, 12 na 79, lingine likifungwa na Mzambia, Kennedy Musonda dakika ya 52, wakati la Tanzania Prisons limefungwa na Beno Ngassa dakika ya tano.
Bingwa wa Ligi Kuu na mshindi wa pili wakifuzu Ligi ya Mabingwa Afrika na mshindi wa tatu na wa nne wakienda Kombe la Shirikisho Afrika.
Aidha, kiungo mshambuliaji Mburkinabe Stephane Aziz Ki akiibuka mfungaji Bora kwa ambao yake 21 mbele ya nyota wa Azam FC, mzawa Feisal Salum Abdallah aliyefunga mabao 19.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo Coastal Union imetoka sare ya bila mabao na KMC Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga, Namungo imeichapa 3-2 Tabora United Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, Mashujaa FC imeichapa Dodoma Jiji 3-0 Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, Ihefu SC imeichapa 5-1 Mtibwa Sugar Uwanja wa LITI mjini Singida na Kagera Sugar imewachapa wenyeji, Singida Fountain Gate 3-2 Jijini Mwanza.
Kwa matokeo hayo, timu za Mtibwa Sugar na Geita Gold zimeipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu, huku Tabora United na JKT Tanzania wakilazimika kumenyana nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atasalia Ligi Kuu, atakayefungwa atakwenda kumenyana na Biashara United iliyofuzu kutoka Championship kujaribu tena kurudi Ligi Kuu.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA