ENGLAND NA HISPANIA ZATINGA ROBO FAINALI EURO 2024
TIMU za England na Hispania zimefanikiwa kutinga Robo Fainali ya Kombe la Mataifa ya Ulaya ‘Euro 2024’ baada ya kuzitoa Slovakia na Georgia jana nchini Ujerumani.
Uwanja wa Arena AufSchalke mjini Gelsenkirchen mchezo ulilazimika kwenda hadi 120 baada ya kiungo wa Real Madrid, Jude Victor William Bellingham kuisawazishia England dakika ya 90’+5 na kufuatia mshambuliaji wa Slavia Prague, Ivan Schranz kuanza kuifungia Slovakia dakika ya 25 na mchezo kuhamia kwenye dakika 30 za nyongeza.
Alikuwa Nahodha na mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Edward Kane aliyeifungia England bao la ushindi dakika ya kwanza tu ya dakika za nyongeza na kuipa tiketi ya Robo Fainali ambako itakutana na Uswisi iliyowatoa mabingwa watetezi, Italia juzi.
Shughuli ilikuwa nyepesi tu Hispania Uwanja wa RheinEnergieStadion Jijini Cologne, kwani licha ya kutanguliwa kwa bao la kujifunga la beki wa Real Sociedad, Robin Le Normand dakika ya 18, mwishowe ilishinda 4-1.
Mabao ya Hispania yalifungwa na viungo, Rodrigo Hernández Cascante ‘Rodri’ wa Manchester City dakika ya 39, Fabián Ruiz Peña wa Paris Saint-Germain dakika ya 51, Nicholas "Nico" Williams Arthuer wa Athletic Bilbao dakika ya 75 na Daniel Olmo Carvajal wa RB Leipzig dakika ya 83.
Hispania sasa watakutana na wenyeji, Ujerumani katika ‘Bonge la Robo Fainali’ Ijumaa Uwanja wa MHPArena Jijini Stuttgart.
Comments
Post a Comment