ITALIA YAIPOKONYA TONGE MDOMONI DAKIKA YA MWISHO EURO 2024
MABINGWA watetezi, italia wamefanikiwa kutinga hatua ya 16 Bora Kombe la Mataifa Ulaya 'Euro 2024' licha ya sare ya 1-1 na Croatia katika mchezo wa Kundi B usiku wa jana Uwanja wa Leipzig Jijini Leipzig nchini Ujerumani.
Kiungo mkongwe wa umri wa miaka 38, Luka Modrić wa Real Madrid alianza kuifungia Croatia dakika ya 55, dakika moja tu tangu mkwaju wake wa penalti uokolewe na kipa Gianluigi Donnarumma.
Lakini mashabiki wa Croatia wakifurahia na kuamini wamesonga mbele, kiungo wa Lazio, Mattia Zaccagni aliwainua mashabiki wa Italia na kuwanyamazisha wapinzani kwa kufunga bao la kusawazisha dakika ya nane na mwisho muda wa nyongeza baada ya kutima dakika 90 za kawaida za mchezo.
Mechi nyingine ya Kundi B jana bao pekee la mshambuliaji wa Barcelona, Ferran Torres García dakika ya 13 liliipa Hispania ushindi wa 1-0 dhidi ya Albania Uwanja wa Dusseldorf Arena Jijini Dusseldorf.
Hispania imeongoza Kundi B kwa pointi zake tisa ikifuatiwa na Italia pointi nne na zote zimefuzu 16 Bora, wakati Croatia yenye pointi mbili na Albania wenye pointi moja wote wanarejea nyumbani.
Ikumbukwe Kundi A timu zilizofuzu ni wenyeji, Ujerumani waliomaliza na pointi saba na Uswisi pointi tano, huku Hungary yenye pointi tatu inakwenda kwenye kapu la washindi wa tatu bora na Scotland yenye pointi moja inarejea nyumbani.
Comments
Post a Comment