SERIKALI YAWAPA TAIFA STARS MILIONI 110 KUIFUNGA ZAMBIA KWAO


WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Daniel Ndumbaro leo amekabidhi Shilingi Milioni 110 kwa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, yote ikiwa zawadi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Waziri Ndumbaro amekabidhi mfano wa Hundi ya Sh. Milioni ambazo Rais Samia aliahidi iwapo Taifa Stars itaifunga Zambia na Fedha taslimu Sh. Milioni ambayo Mheshimiwa Rais hutoa kwa kila bao linalofungwa timu ya Taifa.
Ikumbukwe juzi Taifa Stars iliibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Zambia katika mchezo wa Kundi E kufuzu Kombe la Dunia 2026 uliofanyika Uwanja wa Levy Mwanawasa Jijini Ndola.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee mshambuliaji wa KMC, Waziri Junior Shentembo dakika ya tano akimalizia pası ya kiungo wa Yanga SC, Mudathir Yahya Abbas.
Kwa ushindi huo, Taifa Stars imefikisha pointi sita katika mchezo wa tatu na kusogea nafasi ya pili nyuma ya vinara, Morocco ‘Simba wa Atlasi’ ambao wamecheza mechi mbili, wakati Zambia inabaki na pointi zake tatu za mechi nne nafasi ya nne ikizidiwa tu wastani wa mabao na Niger iliyocheza mechi mbili - na Kongo inashika mkia ikiwa imecheza mechi moja na kufungwa.
Wapinzani wengine katika Kundi E kufuzu Kombe la Dunia 2026 Eritrea walijitoa katika mbio za kuwania tiketi ya Fainali hizo zinazoandaliwa kwa pamoja na Canada, Mexico na Marekani.


Mechi mbili za awali Taifa Stars ilifungwa 2-0 na Morocco nyumbani Novemba 21 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam, kabla ya kushinda 1-0 dhidi ya Niger Novemba 18 mwaka jana Uwanja wa Marrakech nchini Morocco.
Siku hiyo bao pekee la Taifa Stars lilifungwa na mshambuliaji mzaliwa wa DRC, Kokola Charles William M'Mombwa wa Macarthur FC ya Australia.
Mechi zijazo Taifa Stars itacheza mwakani ikianzia nyumbani dhidi ya Kongo Machi 17, kabla ya kwenda ugenini kwa michezo miwili, dhidi ya Morocco Machi 24 na Kongo Septemba 1.
Baada ya hapo Taifa Stars itarejea nyumbani kwa michezo miwili ya mwisho ya Kundi E dhidi ya Niger Septemba 8 na Zambia Oktoba 6 mwakani.
Washindi wa kwanza tisa wa makundi A, B, C, D, E, F, G, H na I watafuzu moja kwa moja Kombe la Dunia 2026, wakati timu nne zitakazomaliza nafasi ya pili na wastani mzuri zitamenyana katika Mchuno kutafuta ya kwenda kwenye mchujo wa Mabara utakaohusisha pia timu za mabara yote kasoro UEFA na nyingine moja kutoka Bara wenyeji, CONCACAF.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA

NYOTA WA SIMBA SC ILIYOFIKA NUSU FAINALI KLABU BINGWA AFRIKA, ABBAS DILUBGA AFARIKI DUNIA