UTURUKI NA GEORGIA NAZO ZAFUZU HATUA YA 16 BORA EURO 2024
TIMU za Uturuki na Georgia zimefanikiwa kufuzu Hatua ya 16 Bora Kombe la Mataifa ya Ulaya ‘Euro 2024’ baada ya ushindi katika mechi zao za Kundi F jana dhidi ya Ureno na Czechia nchini Ujerumani.
Mabao ya winga wa Napoli ya Italia, Khvicha Kvaratskhelia dakika ya pili na mshambuliaji wa Metz ya Ufaransa, Georges Mikautadze dakika ya 57 kwa penalti yaliipa Georgia ushindi wa 2-0 dhidi ya Ureno ya Cristiano Ronaldo Uwanja wa Arena AufSchalke, mjini Gelsenkirchen.
Na mabao ya Uturuki yalifungwa na kiungo wa Inter Milan, Hakan Çalhanoğlu dakika ya 51 na mshambuliaji wa Besiktas, Cenk Tosun dakika ya 90’+4, wakati la Czechia lilifungwa na kiungo wa West Ham United dakika ya 66.
Ureno na Uturuki zote zimemaliza na pointi sita na kwa pamoja na zinafuzu Hatua ya 16 Bora kutoka Kundi F, wakati Georgia imefuzu kama miongoni mwa timu nne zilizomaliza nafasi ya tatu na wastani mzuri zaidi wa pointi.
Mechi za Kundi E zote zilimalizika kwa sare Slovakia 1-1 na Romania na Ukraine 0-0 na Ubelgiji na kwa matokeo hayo timu zote zinamaliza na pointi nne zikitofautiana tu wastani wa mabao.
Romania na Ubelgiji zinafuzu kwa wastani mzuri wa mabao, wakati Slovakia imefuzu kama miongoni mwa timu nne zilizomaliza nafasi ya tatu na wastani mzuri zaidi wa pointi na Ukraine inarejea nyumbani.
Kwa ujumla timu zilizofuzu Hatua ya 16 Bora ni Uswisi, Italia, Ujerumani, Denmark, England, Slovakia, Hispania, Georgia, Ufaransa, Ubelgiji, Ureno, Slovenia, Romania, Uholanzi, Austria na Uturuki na Hatua huyo itaanza Jumamosi.
Mechi za 16 Bora ni Uswisi dhidi ya Italia, Ujerumani na Denmark, England na Slovakia, Hispania na Georgia, Ufaransa na Ubelgiji, Ureno na Slovenia, Romania na Uholanzi na Austria dhidi ya Uturuki.
Comments
Post a Comment