AISHA MASAKA AJIUNGA BRIGHTON & HOVE ALBION YA ENGLAND
KLABU ya Brighton & Hove Albion imemtambulisha mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Aisha Masaka (20) kutoka BK Hacken ya Sweden kuwa mchezaji wake mpya kwa masharti ambayo hayajawekwa wazi, kulingana na taratibu za kawaida za udhibiti.
Mkurugenzi Mkuu wa soka ya wanawake na wasichana wa Brighton & Hove Albion, Zoe Johnson pamoja na kumkaribisha kwa furaha Aisha – pia amemwagia sifa kwamba ni mshambulaji mzuri aliyefanya vizuri katika Ligi ya Sweden na Ligi yaMabingwa Ulaya akiwa na Hacken.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 alijiunga na Hacken mwaka 2022 akitokea Young Africans ‘Yanga Princess’ ya nyumbani, Tanzania baada ya kuibukia Alliance FC ya Mwanza.
Katika misimu miwili aliyokaa Hacken, fowadi huyo aliwasaidia kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Sweden na kuifikisha Robo Fainali ya UEFA Champions League msimu uliopita kabla ya kutolewa na PSG.
Wakati anacheza Tanzania, alikuwa Mfungaji Bora msimu wa 2020/21 akiifungia Young Priness jumla ya mabao 35 katika mechi 20.
Na kwa upande wa timu ya taifa, Aisha ameichezea Twiga Stars jumla ya mechi 15, akiifunga mabao tisa tangu mwaka 2021 alipochaguliwa kwa mara ya kwanza.
Aisha alianzia timu ya wasichana na aling’ara katika michuano ya Kombe la COSAFA kwa mabinti chini ya umri wa miaka 17 akiiwezesha Serengeti Girls kutwaa ubingwa, huku yeye akiwa mfungaji bora.
Aisha ni miongoni mwa wanasoka walioiwezesha Twiga Stars kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa kwa Wanawake (WAFCON) 2024 zitakazofanyika baadaye mwaka huu nchini.
Comments
Post a Comment