AZAM FC YAFUNGA USAJILI KWA SAINI YA KIUNGO WA BELOUIZDAD
KLABU ya Azam FC imemsajili kiungo mkabaji wa Kimataifa wa Mali, Mamadou Samake (24) kwa mkataba wa miaka miwili akitokea CR Belouizdad ya Algeria.
Taarifa ya Azam FC imesema kwamba Mamadou Samake anafunga rasmi usajili wa klabu hiyo katika dirisha hili la mwanzo wa msimu 2024/25.
Taarifa ya Azam FC imesema kwamba Samake atajiunga na kambi ya timu nchini Morocco muda wowote kuanzia sasa, tayari maandalizi ya msimu.
Huyo anakuwa mchezaji mpya wa nane baada ya beki wa kati, Yoro Mamadou Diaby kutoka Stade Malien alipokuwa anacheza kwa mkopo kutoka akademi ya Yeleen Olympique ya Mali na viungo mshambuliaji, Muivory Coast, Franck Tiesse kutoka Stade Malien, kiungo mshambuliaji, Cheickna Diakite (19) kwa mkataba wa miaka mitatu kutoka Real Bamako ya kwao, Mali.
Wengine ni Wacolombia, kiungo Ever Meza kutoka Leonnes ya kwao na mshambuliaji Jhonier Blanco kutoka Aguilas Doradas ya kwao pia, Colombia.
Kuna wazawa pia wawili, kiungo Nassor Saadun Hamoud kutoka Geita Gold na mshambuliaji Adam Omary Adam kutoka Mashujaa ya Kigoma.
Aidha, Azam FC pia imemnunua moja kwa moja na kumsainisha mkataba wa miaka miwili kipa wa Kimataifa was Sudan, Mohamed Mustafa kutoka El Merreikh ya Sudan.
Hatua hiyo inafuatia kazi nzuri ya kipa huyo kufuatia kusajiliwa kwa mkopo mwezi Januari akiisaidia Azam FC kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara na Kombe la CRDB la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Comments
Post a Comment