COASTAL UNION YATOA DROO, SINGIDA YASHINDA KAGAME, LAKINI…
TIMU ya Coastal Union imekamilisha mechi zake za Kundi A Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame kwa kutoa sare ya kufungana bao 1-1 na Hay Al Wadi Nyala ya Sudan Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Mohamed Hasssa alianza kuifungia Al Wahdi dakika ya 48, kabla ya Abdallah Dennis kuisawazishia Coastal Union dakika ya 53.
Mchezo mwingine wa Kundi A, mabingwa wa Zanzibar, JKU wamechapwa mabao 2-1 na Dekedaha ya Somalia jioni ya leo hapo hapo Uwanja wa KMC.
Mabao ya Dekedaha yamefungwa na Joshua Abdalie dakika ya 60 na Adepoju Oluwasen dakika ya 71, wakati bao pekee la JKU limefungwa na Ahmed Hamisi Machano dakika ya nne.
Msimamo wa Kundi A sasa ni Hay Al Wad pointi saba kileleni wakifuatiwa na Coastal Union pointi nne, JKU pointi tatu sawa na Dekedaha.
Mechi za Kundi C zilizochezwa mchana, Singida Big Stars iliibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya El Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini, wakati SC Villa ya Uganda ililazimishwa sare ya 1-1 na APR ya Rwanda.
Mabao ya Singida Big Stars yamefungwa na Marouf Tchakei dakika ya 18, Edmund John dakika ya 43 na Ayoub Lyanga dakika ya 76, wakati bao pekee la El Merriekh Bentiu limefungwa na Jack James dakika ya 47 Uwanja wa Azam Complex.
Olivier Dushimana alianza kuifungia APR dakika ya 30, kabla ya Najib Yiga kuisawazishia SC Villa dakika ya 90’+2 Uwanja wa KMC.
Msimamo wa Kundi C sasa ni APR pointi saba kileleni ikifuatiwa na SC Villa pointi tano, Singida Black Stars pointi tano na El Merriekh Bentiu pointi moja.
Matokeo hayo yanamamışha vinara wa Kundi A, Hay Al Wadi Nyala wamefuzu Nusu Fainali na vinara wa Kundi C APR wakiungana na vinara wa Kundi B, Al Hilal Omdurman ya Sudan.
Timu nyingine itakayofuzu Nusu Fainali ni itakayomaliza na pointi zaidi katika nafasi ya pili kwenye makundi yote baada ya mechi za mwisho za Kundi B kesho.
Comments
Post a Comment