SIMBA SC WAREJEA DAR TAYARI KWA SIMBA DAY JUMAMOSI


KIKOSI cha Simba SC kimerejea nchini jioni ya leo kikitokea Misri ambako kilikuwa kimeweka kambi ya wiki tatu kujiandaa na msimu mpya chini ya kocha wao mpya, Fadlu Davids raia wa Afrika Kusini.
Baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JINIA), eneo la Kipawa Jijini Dar es Salaam – moja kwa moja moja kikosi cha Simba kilikwenda kambini Bunju kwa matayarisho ya mwisho ya tamasha la Simba Day Jumamosi Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini.
Simba Day ni tamasha maalum kwa klabu hiyo kutambulisha kikosi cha msimu mpya pamoja na benchi la Ufundi, ambalo hutanguliwa na burudani mbalimbali ikiwemo muziki na Jumamosi hii litahitimishwa kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya APR ya Rwanda.
Ikiwa kambini mjini Ismailia nchini Misri – Simba Sports Club ilipata mechi tatu za kujipima nguvu na kushinda zote, 3-0 dhidi ya El-Qanah Julai 22 na 2-1 mara mbili, dhidi ya Telecom Egypt Julai 28 na dhidi ya Al-Adalah FC ya Saudi Arabia Julai 29.
Baada ya tamasha la Simba Day, Wekundu hao wa Msimbazi watarejea kambini kujiandaa na mchezo wa Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya watani, Yanga Agosti 8 Uwanja wa Mkapa.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA