WAZIRI MKUU MAJALIWA APONGEZA UWEKEZAJI MKUBWA AZAM MEDIA KWENYE MICHEZO


WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa jana ameipongeza Kampuni ya Azam Media Limited kwa kuisaidia Tanzania kupata vigezo vya kuwa wenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifaya Afrika (AFCON) mwaka 2027.
Waziri Mkuu, Majaliwa aliyasema hayo jana wakati wa hafla ya Azam Media Limited kuzindua vifaa vipya na vya kisasa vya kurushia matangazo ya mpira pamoja na mashine za Msaada wa Picha za Video kwa Marefa (VAR), shughuli ambayo ilifanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu huyo amelishauri Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Azam Media kupitia na kuboresha mikataba yake ya udhamini na Azam Media Limited ili kuwapa uhakika juu ya uwekezaji wao wa Mabilioni ya Fedha.
Kwa ujumla Waziri Majaliwa ameipongeza Azam Media kwa kukukuza sekta ya michezo kwa ujumla kutokana na kuonyesha michezo mingi kwenye Televisheni yake mbali na soka - ikiwemo ndondi na mpira wa kikapu.  
"Tumekutana hapa kwa ajili ya kushuhudia tukio la kihistoria...nasema ni la kihistoria kwasababu hatujawahi kupata chombo cha habari chenye uwingi wa vifaa vya majukumu yake kama Azam Media." alisema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Mapema Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited, Divisheni ya Maudhui, Patrick Kahemele alisema wameongeza Chaneli mpya, Azam Sports 4 HD ambayo Waziri Mkuu, Majaliwa aliizindua.
Shughuli hiyo ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma 'Mwana FA', Katibu wa Wizara hiyo, Gerson Msigwa pamoja na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia.
Walikuwepo viongozi wengine mbalimbali wa Serikali, Vyama na Mashirikisho ya Michezo pamoja na viongozi na wafanyakazi wa Bakhresa Group Limited, wamiliki wa Azam Media.
Mei 25, mwaka 2021 Kampuni ya Azam Media iliingia mkataba wa miaka 10 na TFF kuanzia msimu 2021-2022 wenye thamani ya Shiling za Tanzania Bilioni 265, shughuli ambayo ilifanyika katika hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam.
Historia ya ushirika wa Azam Media na TFF inanzia Agosti 30 mwaka 2013 waliposaini mkataba wa kwanza wa haki za Matangazo ya Televisheni kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu uliokuwa na thamani ya Sh. Bilioni 5.5 (5,560,800,000), shughuli ambayo ilifanyika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA