CHANGALAWE AMTWANGA BINGWA WA AFRIKA MKONGO KABEJI ADDIS ABABA


BONDIA Yusuf Changalawe amefanikiwa kushinda pambano lake la usiku wa kuamkia leo na kufuta uteja mbele ya Bingwa wa Afrika Pita Kabeji kutoka DR Congo katika mapambano ya Usiku wa Mabingwa wa IBA yaliyofanyika katika ukumbi wa makumbusho wa Adwa, Mji mkuu wa Afrika Addis Ababa, Ethiopia. 
Pambano hilo lililokuwa na mvuto zaidi kati ya miamba hao wa Afrika katika uzani wa Light heavyweight 80kg, lilikuwa la tatu kukutana huku Changalawe akipoteza mara 2 dhidi ya Kabeji katika hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Afrika Accra - Ghana 2023 na katika fainali ya mashindano ya Mandela Durban 2024 kwa matokea ya kutenganisha (Split decision)
Changalawe aliyecheza kwa ustadi wa hali ya juu na kutumia akili nyingi alishinda kwa matokeo ya kutenganisha (split decision) katika pambano hilo la round nane (8) huku akishangiliwa zaidi na Waethiopia waliovutiwa na mchezo wake.
"Ninamshukuru Mungu kwa ushindi wa leo, Nawashukuru IBA, AFBC na BFT kwa kunipa nafasi hii, hakika nimetimiza ndoto yangu ya kulipiza kisasa kwa Kabeji" alinukuliwa Changalawe baada ya pambano. 
Usiku wa Mabingwa wa IBA ni matamasha ya ngumi yanayozunguka Duniani na hili la Addis Ababa likiwa la kwanza kufanyika katika bara la Afrika huku dhima kuu ikiwa kuwajengea uwezo mabondia wa ridhaa kwenye ngumi za kulipwa na kuwainua kiuchumi.
Changalawe aliambatana na Mwalimu Mkuu wa Timu ya Taifa "Faru Weusi wa Ngorongoro" Samwel "Batman" Kapungu akisaidiana Katibu Mkuu Makore Mashaga. 
"Tunashukuru kwa ushindi huu, tunaushukuru Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Watanzania wote waishio Addis Ababa na wenyeji WaEthiopia waliojitokeza kutuunga mkono na kutushangilia" alinukuliwa Raisi wa Shirikisho la Ngumi Tanzania Ndg. Lukelo Willilo.
Timu inatarajiwa kusafiri asubuhi ya leo kurejea Dar es salaam kwa usafiri wa Shirika la Ndege la Ethiopia na kuwasili majira ya saa 7:45 mchana.
Changalawe (kulia) akishangilia baada ya kutangazwa mshindi dhidi ya Bingwa wa Afrika Pita Kabeji kutoka DR Congo (Kushoto)


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA