MAHOJIANO BIN ZUBEIRY NA NICO NJOHOLE

ALIZALIWA Desemba 12, mwaka 1960, eneo la Chang’ombe Jijini Dar es Salaam, kabla ya kupata elimu yake ya Msingi katika shule ya Msimbazi Wavulana, baadaye sekondari ya Kinondoni Muslim Kidato cha kwanza pekee, akahamia Forodhani alikosoma hadi Kidato cha Nne.
Wakati huo tayari alikwishakuwa mwanasoka maarufu kwenye vitongoji vya Jiji, akianzia timu za mitaa aliyoishi Chang’ombe na Ilala, baadaye Msimbazi Rovers ‘Pentagon’, kabla ya kujiunga na timu ya vijana ya Simba, maarufu kama Simba B.
Kufuatia kundi kubwa la nyota wa Simba kutimkia Uarabuni wakiwemo viungo Haidari Abeid na Khalid Abeid, akawa miongoni mwa chipukizi waliopandishwa kikosi cha kwanza mwishoni mwa mwaka 1977 – wengine ni George Kulagwa, Rahim Lumelezi, Abbas Kuka.
Alicheza Simba kwa mafanikio hadi mwaka 1982 alipoamua kwenda kucheza soka ya kulipwa Ulaya, akianzia England ambako pamoja na kukubalika kwenye klabu za AFC Bournemouth na Arsenal lakini ugumu wa kupata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa, ITC ulimkwamisha.
Ndipo alipoamua kwenda Austria ambako wanasoka wengine wa Tanzania, Sunday Manara na mdogo wake, Kassim Manara walitangulia na kufanikiwa kupata timu – naye akafanikiwa kupata timu, hivyo kufungua ukurasa mpya wa maisha yake ya kisoka Ulaya.
Alianzia SV Wernberg mwaka 1982 kabla ya kuhamia Asko Furnitz, zote zikiwa Daraja la Tatu ambayo aliichezea hadi mwaka 1992 aliporejea nyumbani na kujiunga tena na Simba akaichezea kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.
Ilipomalizika michuano hiyo, akarejea Ulaya na kujiunga tena na Asko Furnitz aliyoichezea hadi mwaka 1998 alipoamua kustaafu soka.
Yeye alifungua milango ya wadogo zake katika soka na klabu ya Simba kwa ujumla, beki Deo na kiungo Renatus wote wakiwa watoto wa Kanali Mstaafu wa JKT, marehemu Boniface Njohole. 
Nicodemus Boniface Njohole pia amecheza timu ya taifa kati ya mwaka 1981 na 1982. 


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA