RAIS WA ZAMANI WA CAF ISSA HAYATOU AFARIKI DUNIA
RAIS wa zamani wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Mcameroon Alhaj Issa Hayatou, amefariki dunia jana Jijini Paris nchini Ufaransa akiwa na umri wa miaka 77.
Rais wa Shirikisho la Soka Cameroon (FECAFOOT), Samuel Eto'o amesema leo kwamba Hayatou amefariki Saa 24 kabla ya kutimiza miaka 78 kufuatia kuugua nchini humo.
Mapema jana Rais wa FIFA, Gianni Infantino alitoa taarifa za kifo cha Hayatou kupitia ukurasa wake wa Instagram: "Nimehuzunishwa kusikia kifo cha rais wa zamani wa CAF, rais wa zamani wa FIFA na muda mfupi, makamu wa rais wa FIFA na mjumbe wa Baraza la FIFA Issa Hayatou,".
"Akiwa shabiki wa michezo, alijitolea maisha yake kwa michezo. kwa niaba ya FIFA, rambirambi ziende kwa familia yake, marafiki, wafanyakazi wenzake wa zamani na wote wanaomfahamu wapumzike kwa amani,".
Hayatou pia alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) kwa miaka 15, hadi 2016, na alibaki kuwa Mjumbe wa heshima.
Ingawa alikuwa mwanariadha nyota enzi zake, lakini ni soka ambayo Hayatou ilimpatia umaarufu na kumjengea heshima zaidi kutokana na uongozi wake CAF alipochaguliwa mwaka 1988 na miaka minne baadaye akachagulwa kuwa Makamu wa Rais wa FIFA.
Mwaka 2002, wakati wa msukosuko mkubwa wa kifedha na kisiasa katika FIFA, Hayatou aliwania Urais wa FIFA dhidi ya Rais wa wakati huo, Sepp Blatter akiungwa mkono zaidi na mataifa ya Ulaya, japo alishindwa akiambulia kura 56 dhidi ya 139 za Blatter ambaye aliendelea kuongoza hadi mwaka 2015 alipoondolewa kwa kashfa ya ufisadi.
Hayatou alikaimu Urais wa FIFA kwa miezi minne kuelekea uchaguzi mwingine uliomuweka madarakani Infantino na mwaka 2017, utawala wa miaka 29 wa Hayatou ulifikia tamati CAF baada ya kushindwa na Ahmad Ahmad wa Madagascar aliyekuwa akiungwa mkono na Infantino.
Mwaka 2021 Hayatou alifungiwa kujihusisha na soka kwa mwaka mmoja kwa madai ya kukiuka "wajibu wa uaminifu" katika mkataba wa haki za kibiashara katika CAF.
Katika kesi nyingine, alikaripiwa na tume ya maadili ya IOC mwaka wa 2011 kwa kuchukua malipo ya Fedha taslimu kutoka kwa wakala wa uuzaji wa Uswisi, ISL, mnamo 1995 ilipouza haki za utangazaji za Kombe la Dunia kwa FIFA.
Hayatou alizaliwa Agosti 9, mwaka 1946 mjini Garoua katika familia mashuhuri ya Cameroon, na kaka yake Sadou alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya kitaifa mnamo 1991-92.
Hayatou alikuwa mchezaji wa timu za taifa za mpira wa Kikapu na Riadha za Cameroon na anashikilia rekodi ya mbio za mita 400 na 800.
Mungu ampumzishe kwa amani.
Comments
Post a Comment