YANGA SC YAICHAPA VITAL'O 6-0, KUCHEZA NA WAHABESHI KUWANIA MAKUNDI
MABINGWA wa mataji yote Tanzania, Yanga SC wamefanikiwa kufuzu Hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Vital’O ya Burundi katika mchezo wa marudiano Raundi ya Awali Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga leo yamefungwa na kiungo Muivory Coast, Peodoh Pacome Zouzoua dakika ya 14 kwa penalti, mshambuliaji mzawa, Clement Francis Mzize dakika ya 49, kiungo Mzambia Clatous Chota Chama dakika ya 51, mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Dube Mpumelelo na viungo, Mburkinabe Stephane Aziz Ki dakika ya 78 na Mudathir Yahya Abbas dakika ya 86.
Yanga inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 10-0, kufuatia kuichapa Vital'O 4-0 kwenye mchezo wa kwanza hapo hapo Azam Complex Jumamosi iliyopita, mabao ya Dube dakika ya sita, Chama dakika ya 68, dakika ya 74 na Aziz Ki kwa penalti dakika ya 90'+1.
Sasa Yanga itakutana na CBE (Benki ya Biashara Ethiopia) ambayo imeitoa SC Villa ya Uganda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Uwanja wa Mandela, Namboole Jijini Kampala wiki iliyopita, kabla ya sare 1-1 leo Abebe Bikila Jijini Addis Ababa.
Yanga wataanzia ugenini Septemba 13, kabla ya kurejea Dar es Salaam kwa mchezo wa marudiano Septemba 20 kusaka tiketi ya hatua ya makundi.
Comments
Post a Comment