AZAM FC YAANZA LIGI,YAIKUNG'UTA KMC MABAO 4-0 MWENGE


TIMU ya Azam FC imeichapa KMC mabao 4-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania uliofanyika Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Azam FC yamfungwa na winga Iddi Suleiman Nado dakika ya 19, beki Lusajo Elukaga Mwaikenda  dakika ya 55, mshambuliaji Nassor Saadun Hamoud dakika ya 60 na beki Freddy Tangalu aliyejifunga dakika ya 67.
Huo unakuwa ushindi wa kwanza kwa Azam FC msimu huu baada ya kutoa sare za bila mabao katika mechi zake zilizotangulia dhidi ya JKT Tanzania Agosti 28 na Pamba Jiji Septemba 14 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Kwa KMC hicho kinakuwa kichapo cha pili msmu huu baada ya awali kufungwa 2-1 na Singida Black Stars Uwanja wa CCM Liti mjini Singida Septemba 12, wakati mechi nyingine wametoa droo ya 1-1 na Coastal Union Agosti 29 Uwanja wa nyumbani na kushinda 1-0 dhidi ya Ken Gold Septemba 16 Uwanja wa KMC.
Kiungo Feisal Salum aliyakabidhiwa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi baada ya mchezo huo kutokana n kiwango kizuri alichoonyesha leo. 


Ligi Kuu itaendelea kesho mechi mbili zaidi, Tabora United wakiwakaribisha Fountain Gate kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora na Kagera Sugar wakiwa wenyeji wa Ken Gold kuanzia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Tabora United na Fountain Gate kila moja ina pointi saba baada ya wote kucheza mechi nne, wakati Kagera Sugar ina pointi moja iliyovuna katika mechi nne na Ken Gold imepoteza mechi zake zote tatu za awali.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA