TAIFA STARS YAAMBULIA SULUHU KWA ETHIOPIA LEO DAR KUFUZU AFCON


TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeanza kwa sare ya bila mabao na Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa Kundi F kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) usiku huu Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Suluhu hiyo inamaanisha Taifa Stars wamekosa zawadi ya Sh. Milioni 20, ahadi ya klabu za Azam, Simba na Yanga kama wangeshinda kuanzia mabao matatu na 5 nyingine kutoka kwenye mfuko wa Goli la Mama, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Mechi ya pili ya Kundi F itafuatia Ijumaa kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuwa wenyeji wa Guinea kuanzia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Martyrs de la PentecĂ´te Jijini Kinshasa.
Mechi za pili za Kundi hilo Ethiopia watakuwa wenyeji wa DRC Septemba 9 hapa hapa Mkapa, wakati Taifa Stars watawafuata Guinea Septemba 10 mechi ambayo itachezwa Uwanja wa Charles Konan Banny de Yamoussoukro mjini Yamoussoukro nchini Ivory Coast.
Jumla ya nchi 52 zinatarajiwa kushiriki hatua ya makundi ya kuwania tiketi ya AFCON 2025 kuanzia Septemba 2 hadi Novemba 19 mwaka huu na washindi wawili wa makundi yote 12 watatengeneza idadi ya timu 24 wakiwemo wenyeji Morocco, kufuzu AFCON ya mwakani.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA