TAIFA STARS YAANZA RASMI KUWANIA TIKETI YA AFCON 2025


TIMU ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars leo imeweka hai matumaini ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Guinea katika mchezo wao wa pili wa Kundi H Uwanja wa Charles Konan Banny de Yamoussoukro nchini Ivory Coast.
Haukuwa ushindi mwepesi kwa Taifa Stars, kwani ililazimika kutokea nyuma baada ya mshambuliaji wa Lille ya Ufaransa, Mohamed Lamine Bayo kuanza kuwafungia Guinea dakika ya 57.
Lakini nyota wa Azam FC, Feisal Salum Abdallah akaisawazishia Tanzania dakika ya 61, kabla ya kiungo mwenzake, Mudathir Yahya Abbas wa Yanga kufunga bao la ushindi dakika ya 88.
Matokeo hayo yanaibakisha Taifa Stars nafasi ya pili ikifikisha pointi nne, nyuma ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yenye pointi sita, wakati Guinea inaendelea kushika mkia nyuma ya Ethiopia yenye pointi moja.
Tanzania ilianza kwa kusuasua kampeni za kuwania tiketi ya AFCON ya mwakani nchini Morocco baada ya kulazimishwa sare ya bila mabao na Ethiopia Jumatano Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wao, Guinea mechi ya kwanza walichapwa 1-0 na DRC Ijumaa Uwanja wa Martyrs de la Pentecôte Jijini Kinshasa.
Ikumbukwe DRC jana waliendeleza wimbi la ushindi baada ya kuichapa Ethiopia 2-0, mabao ya kiungo wa Spartak Moscow, Théo Bongonda Batombo dakika ya 62 na mshambuliaji wa Pyramids, Fiston Kalala Mayele dakika ya 76 Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Jumla ya nchi 52 zinashiriki hatua ya makundi ya kuwania tiketi ya AFCON 2025, mchuano ulioanza mwanzoni mwa mwezi huu na utaendelea hadi Novemba 19 mwaka huu – na washindi wawili wa makundi yote 12 watatengeneza idadi ya timu 24 wakiwemo wenyeji Morocco katika Fainali za AFCON ya mwakani.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA