TAIFA STARS YACHAPWA 2-0 NA DRC UWANJA WA MKAPA KUFUZU AFCON
TANZANIA imejiweka njia panda katika mbio za kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2025 baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC katika mchezo wa Kundi H Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam leo.
Mabao yaliyoizamisha Taifa Stars leo yamefungwa na nyota wa Young Boys ya Uswisi, Meschack Elia Lina akimalizia pasi za washambuliaji wenzake, Nathanael Mbuku wa Dinamo Zagreb ya Croatia dakika ya 87 na Fiston Kalala Mayele wa Pyramids ya Misri dakika ya 90 na ushei.
Matokeo hayo yanamaanisha Chui wa DRC wenye pointi 12 sasa – wamejikatia tiketi ya AFCON ya mwakani nchini Morocco ikiwa na mechi mbili mkononi dhidi ya Guinea ugenini na Ethiopia nyumbani.
Tanzania inayobaki na pointi zake nne za mechi nne – inaendelea kushika nafasi ya pili mbele ya Guinea yenye pointi tatu na Ethiopia yenye pointi moja baada ya wote kucheza mechi tatu.
Mechi nyingine ya Kundi H itachezwa usiku huu kuanzia Saa 4:00 Uwanja wa Olimpiki Alassane Ouattara Jijini Abidjan nchini Ivory Coast baina ya Ethiopia na Guinea.
Mechi ya kwanza baina ya timu hizo, Guinea walishinda 4-1 hapo hapo Olimpiki Alassane Ouattara – mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Serhou Yadaly Guirassy akipiga hat trick.
Mechi mbili za mwisho Taifa Stars itawafuata Ethiopia, kabla ya kurejea nyumbani kumalizia na Guinea kuangalia hatma yake ya kufuzu Fainali hizo.
Mchezo wa leo ulihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wengine mbalimbali.
Comments
Post a Comment