TANZANIA YAFUZU AFCON U20 BAADA YA KUITOA UGANDA MICHUANO YA CECAFA


TANZANIA imekata tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Uganda katika mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA U20 leo Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge Jijini Dar es Salaam.
haukuwa ushindi mwepesi kwa Ngorongoro Heroes inayofundishwa na Kocha mzoefu, Charles Boniface Mkwasa anayesaidiwa na Kally Ongala na Juma Kasema kocha wa makipa - kwani ililazimika kutoka nyuma baada ya beki Brian Toto Majub kuanza kuifungia Hippos dakika ya 46.
Winga wa KVZ ya Ligi Kuu ya Zanzibar, Sabri Dahary Kondo aliirejesha mchezoni Ngorongoro kwa bao lake zuri la kusawazisha dakika ya 73 ambalo lilisindikizwa nyavuni na kipa wa Hippos, Abdu Magada na dakika 90 zikamalika timu hizo zikiwa zimefungana 1-1.
Shujaa wa Tanzania leo ni mshambuliaji wa JKU ya Ligi Kuu ya PBZ Zanzibar, Jammy Suleiman Simba aliyeifungia Ngorongoro Heroes bao la ushindi dakika ya 119 na kuamsha shangwe kubwa kwa mamia ya mashabiki waliojitokeza Uwanja wa KMC.
Nusu Fainali nyingine ya CECAFA U20 inafuatia Saa 12:00 jioni Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na mshindi pamoja na kwenda Fainali kama Ngorongoro Heroes, pia atafuzu AFCON U20.



Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA