KALI ONGALA KOCHA MPYA KMC


KLABU ya KMC imemtambulisha Kalimangonda Muingereza mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), mwenyeji wa Tanzania - Sam Daniel Ongala kuwa kocha wake mpya Mkuu.
“Tunayo furaha kuwatangazia wakazi wa Kinondoni na wadau wa mpira nchini kwamba tumeingia mkataba na kocha Kali Ongala kuifundisha timu yetu ya KMC Football Club,” imesema taarifa ya KMC.
Ongala anachukua nafasi ya Mmarekani mwenye asili ya Somalia, Abdihamid Moalin aliyeacha kazi baada ya misimu miwili ya kuwa na timu hiyo.
Taarifa ya KMC imesema kwamba imejiridhisha na Ongala kikao kilichopitia wasifu (CV) wa makocha mbalimbali wakiamini ndiye Kocha anayeendana na falsafa ya klabu yao. 
“Uongozi wa klabu ya KMC unamtakia mafanikio Kocha Kali Ongala katika kipindi chote atochohudumu kama kocha ndani ya klabu yetu,” imesema taarifa hiyo.
Kali aliyezaliwa Jijini London, Uingereza Agosti 31 mwaka 1979 amekulia Dar es Salaam ambako wazazi wake walikuwa wanafanya kazi, baba yake Ramazani Mtoro Ongala ‘Dk Remmy’ alikuwa mwanamuziki kutoka DRC na mama yake, Toni alikuwa Mwalimu.
Kabla ya kuwa kocha, Kali alicheza soka pia akiibukia Abajalo ya Sinza hadi mwaka 1999 akasajiliwa Yanga aliyoichezea hadi mwaka 2000 akaenda Marekani chini ya kampuni ya Kajumulo World Soccer kwa lengo la kutafutiwa timu ya kuchezea, yeye pamoja na wachezaji wengine wawili nyota wa Tanzania wakati huo, kiungo mwenzake Salvatory Edward aliyekuwa Yanga pia na mshambuliaji Nteze John, aliyekuwa Simba.
Hata hivyo baadae wote walirejea kuchezea timu ya Kajumulo WS katika ligi ya Tanzania, kabla kuamua kuachana na Mkurugeni wa kampuni hiyo, Alexander Otaqs Kajumulo na kwenda kutafuta usimamizi mwingine.
Kali alikwenda kufanya majaribio na kucheza kwa muda Uingereza na Jamaica kabla ya kujiunga na 
Väsby United mwaka
2005 hadi 2007 akahamia GIF Sundsvall hadi 2010 alipojiunga na 
Umeå FC, zote za Sweden.
Mwaka 2010 alirejea nyumbani na kujiunga na timu ya Azam FC alikocheza hadi 2011 na kustaafu na moja kwa moja kuingizwa kwenye benchi la Ufundi kama Kocha Msaidizi chini ya Muingereza mwenzake, Stewart Hall.
Kwa wakati tofauti Kali amewahi kuwa Kaimu Kocha Mkuu Azam FC na kuna wakati alifundisha Maji Maji ya Songea.
Kwa sasa anajiunga na KMC akiwa Kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes ambayo Kocha wake Mkuu ni Charles Boniface Mkwasa.
Hapana shaka mafanikio ya kuiwezesha Ngorongoro Heroes kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA U20) hivyo kukata tiketi ya kucheza Fainali za Afrika (AFCON U20) yamechangia ushawishi kwa KMC kumchukua.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA