RAIS DK SAMIA AWAZAWADIA TAIFA STARS SH MILIKONI 700 KUFUZU AFCON
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ameizawadia timu ya soka ya taifa ya Tanzania Shilingi Milioni 700 kwa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Morocco.
Taifa Stars ilikata tiketi ya AFCON 2025 baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Guinea jana katika mchezo wa mwisho wa Kundi H Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Zawadi hiyo iliwasilishwa jana mara tu baada ya mchezo na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro uwanjani hapo na Nahodha Mbwana Samatta akatoa shukarni kwa niaba ya wachezaji wenzake.
Pamoja na zawadi hiyo, kupitia ukurasa wake wa Instagram Rais Dk. Samia aliandika jana;
"Tukiwa katika majonzi na kazi ikiendelea katika kuwatafuta ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai kufuatia kuporomoka kwa jengo eneo la Kariakoo, ninawapongeza vijana wetu Taifa Stars kwa ushindi na kufuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025. Mmeandika historia kwa Taifa letu, ikiwa ni mara yetu ya nne kufikia mafanikio haya makubwa katika kipindi cha zaidi ya miaka arobaini.
Hongera kwa kazi nzuri nyote tuliowapa dhamana kusimama na vijana wetu kukamilisha jukumu hili katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Benchi la Ufundi na Watanzania wote kwa kuendelea kuipenda, kuithamini na kuipa hamasa Timu ya Taifa.
Baada ya ushindi huu, sasa tujikite katika maandalizi mazuri zaidi kwa mashindano yajayo,".
Bao pekee la Taifa Stars jana lilifungwa na mshambuliaji wa Al Talaba ya Iraq, Simon Happygod Msuva dakika ya 61 akimalizia pasi nzuri ya kiungo wa Yanga ya nyumbani, Dar es Salaam, Mudathir Yahya Abbas.
Kwa ushindi huo, Taifa Stars imemaliza na pointi 10 na kuungana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliyomaliza na pointi 12, Guinea iliyomaliza na pointi tisa nafasi mbele ya Ethiopia iliyoshika mkia kwa pointi zake nne.
Hii inakuwa mara ya nne kihistoria Tanzania kufuzu AFCON baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria, 2019 Misri na 2023 nchini Ivory Coast na mara ya kwanza kufuzu Fainali mbili mfululizo.
Ikumbukwe kwa tiketi ya uenyeji wakishirikiana na Kenya na Uganda – Tanzania pia watacheza Fainali za AFCON za mwaka 2027.
Comments
Post a Comment