RAMOVIC WA TS GALAXY AFRIKA KUSINI NDIYE KOCHA MPYA WA YANGA
MJERUMANI mwenye asili ya Bosnia and Herzegovina, Sead Ramovic (45) ndiye kocha mpya wa mabingwa wa Tanzania, Yanga anayechukua nafasi ya Muargentina Miguel Angel Gamondi aliyefukuzwa baada ya msimu mmoja na nusu kazini.
Ramovic anajiunga na Yanga akitokea TS Galaxy ya Afrika Kusini, klabu yake ya kwanza kufundisha kama Kocha Mkuu baada ya kustaafu soka mwaka 2014.
Alizaliwa wa Stuttgart, Ujerumani Magharibi na kisoka aliibukia FC Feuerbach kama kipa, kabla ya kuhamia SpVgg Feuerbach mwaka 1995, Stuttgarter Kickers mwaka 1999, VfL Wolfsburg mwaka 2001 na mwaka 2004 alijiunga na Borussia Mönchengladbach alikocheza hadi 2005 akahamia Kickers Offenbach.
Julai 2006 alijiunga na Tippeligaen Tromsø IL ya Norway hadi 2010 akaenda kudakia Sivasspor ya Uturuki hadi 2011 akahamia Metalurh Zaporizhzhia ya Ukraine kwa muda mfupi kabla ya kutimkia FK Novi Pazar ya Serbia.
Novemba 17 mwaka 2011 alijiunga na Lillestrøm SK ya Norway kwa ajili ya msimu wa 2012 kabla ya kuhamia Vendsyssel ya Denmark msimu wa 2013, baadaye Strømsgodset ya Norway pia kabla ya kustaafu Mei 21 mwaka 2014.
Ramović aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Bosnia na Herzegovina mwaka wa 2004 na kujumuika kikosini mara kadhaa, japokuwa hakuwahi kudaka hata mechi moja.
Amekuwa akiifundisha TS Galaxy yenye maskani yake Kameelrivier, Manispaa ya Nkangala jirani na Siyabuswa, Mpumalanga tangu mwaka 2021 na baada ya msimu uliopita kuiwezesha kumaliza nafasi ya sita ambayo ni rekodi kwa klabu hiyo - anahamia Yanga yenye maskani yake makutano ya Mitaa ya Twiga na Jangwani, Kariakoo, Ilala Jijini Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment